Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya ametoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Wilaya kupitia mwa mtendaji kata ya Chikuyu kuboresha miundombinu ya barabara ya kuingilia katika mnada wa Mwiboo kutokana na hali yake kuwa hairidhishi.
Dkt. Chaya ameyasema hayo Julai 17 , 2023 wakati alipofanya ziara katika kata ya Chikuyu vijiji vya Mwiboo, Chilejeho, Mtiwe na Chikuyu iliyokuwa na dhima ya kufanya mikutano ya hadhara, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi hao.
"Hii barabara haipo chini ya TARURA inatakiwa ikarabatiwe na Halmashauri, Mtendaji wa kata kila mnada unakuja kukusanya Mapato lakini hamuikumbuki ili hali ndiyo inayowapa kipato, wakati wa mvua magari hayaingii hapa, Nakuagiza kwa Mkurugenzi wako wa Wilaya tunampa mpaka mwezi wa kumi mwaka huu atume timu yake ifanye tathmini na kutenga fedha kwaajili ya kuweka vifusi kwenye hiyo barabara" Dkt. Chaya.
Akiwa katika mwendelezo wa ziara yake suala la Skimu za umwagiliaji ikaonekana kuwa changamoto kwa wananchi hao ndipo Mbunge huyo akatoa siku saba kwa Mtendaji wa kata ya Chikuyu awe ametoa majina ya wakulima wenye mashamba ya skimu.
Kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) Ameagiza viongozi wanaohusika kutekeleza mpango huo kuhakikisha wanaandikisha majina ya walengwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ili kuchukua hatua zitakazowanufaisha walengwa hao.
Aidha ametoa rai kwa walimu na uongozi wa shule kuwa ni marufuku kumtoa mwanafunzi darasani kama mzazi hajatoa mchango na ikiwezekana iundwe kamati ya wazazi ya kufuatilia michango hiyo na siyo waalimu kwani itakuwa ni njia rahisi ya kuwafikia wazazi hao.
"Kuanzia leo ni marufuku kumrudisha mtoto nyumbani kama hajatoa mchango" ,Dkt. Chaya.
Dkt. Chaya katika mikutano yake hakuacha kuishukuru serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji w miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo la Manyoni Mashariki.
Hata hivyo Mbunge huyo ataendelea ataendelea na Ziara mpaka atakapomaliza kutembelea kata zote zote 19 zilizomo Jimboni humo ambayo itaambatana na Mikutano ya hadhara.
Social Plugin