Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KISHINDO OPARESHENI MAALUM ‘TOKOMEZA MIRUNGI’, HEKARI 535 ZATEKETEZWA KILIMANJARO

Na DCEA - Kilimanjaro

Hekari 535 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa katika oparesheni maalum ‘Tokomeza Mirungi’, iliyoanzia kutekelezwa ndani ya vijiji vya Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande, WIlayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro .


Oparesheni hiyo inafanywa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikishirikiana kwa karibu na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama likiwamo Jeshi la Polisi Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema katika oparesheni hiyo jumla ya watuhumiwa saba wamekamatwa.

Amesema mirungi ni mojawapo ya dawa za kulevya zilizokatazwa nchini kwani ina athari nyingi kwa binadamu, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiafya.

“Inasababisha saratani ya koo, utumbo na uraibu, mtindio wa ubongo, kiuchumi inasababisha nchi inakosa mapato kwa sababu wengi wanaolima mirungi Kata hii na eneo hili la Same hawaingizii mapato yoyote Serikali,” amesema.

“Lakini pia tunahakikisha kwamba kwenye mikataba ya kimataifa ambayo tuliingia mwaka 1961, 1971 na 1986 inatutaka nchi yoyote iliyoingia ile mikataba ihakikishe inafanya oparesheni katika maeneo yake yote.

“Ili kuhakikisha kwamba inatokomeza kabisa suala la dawa za kulevya katika nchi husika, pia lazima ioneshe juhudi inazofanya katika kutokomeza dawa za kulevya kwa wananchi na jamii nzima.

“.., na dunia iweze kuona kuwa kazi inayofanywa na nchi husika katika kutokomeza dawa za kulevya",amesema.

Kamishna Lyimo amesema kwa sababu hiyo ndiyo maana DCEA imepiga kambi mkoani humo kwa ajili ya oparesheni hiyo kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Dola.


Amesema hekari hizo zimeteketezwa kwa muda wa siku nane kuanzia Julai 2 hadi 9, mwaka huu.

“Kwa hiyo niwashukuru wote ambao tunashirikiana nao katika oparesheni hii, tuwaombe wananchi wote kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi wote wa Serikali, mkoa, wilaya, vijiji na Kata.

“Tushirikiane kuhakikisha tunatokomeza dawa za kulevya, mashamba yote hususan katika eneo hili la Wilaya ya Same, lakini pia tuhakikishe kwamba tunaijengea Serikali uwezo wa kuweza kufanya shughuli zake.",amesema.

Kamishna Lyimo amesisitiza “Tumekuja eneo hili tumeona Serikali ilivyojenga miundombinu, maji yapo ya kutosha, imeweka miundombinu ya umeme, barabara inatumia kodi za watu wengine kuja kuweka miundombinu huku.

“Wakati huku wao wanalima mirungi na hawaingizii Serikali Pato lolote na madhara yanayopatikana kwa wananchi, kwa jamii na mtu mmoja mmoja ni mzigo kwa Serikali pia.

Ameongeza “Tumeona hekari nyingi imetushangaza, hatukutegemea kuna hekari kubwa kiasi hiki hadi tunachukua vikosi vya Jeshi JKT kuja kufanya oparesheni hii na kununua mashine za kuteketeza kutokana na ukubwa wa hili eneo.

Amesema , kesho (Jumatatu}, tutakuwa na mkutano mkubwa ili kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya kilimo cha mirungi, ili waweze kuacha kilimo hiki na kwenda kulima kilimo mbadala.

Ameiasa jamii yote kwa ujumla, viongozi wa dini, kimila, Serikali kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na mkoa wote kushirikiana na DCEA kutokomeza biashara ya dawa za kulevya.

“Tanzania inawezekana kuwa salama kwa kutokuwa na dawa za kulevya, Sheria pia imetutaka kwamba ukishakamata shamba limelima dawa za kulevya inaruhusu kutaifisha shamba hilo,.

“Tuiombe jamii tukishaanza kutaifisha mashamba yao, watakosa hata maeneo ya kulima, kuanzia sasa tutaanza kuitekeleza, tukikuta shamba lako limelima bangi, mirungi tunataifisha.

“.., na mali zote zilizopatikana kwa kilimo hicho zinataifishwa kwa hiyo tuwaombe wananchi wasije wakaingia kwenye wimbi la umaskini, waachane kabisa na dawa za kulevya,” ametoa rai.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com