Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba
*Yasema mafanikio hayo yamechangiwa na Serikali ya awamu ya sita kuvutia wawekezaji
Na MWANDISHI WETU
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepata faida ya zaidi ya shilingi trilioni 1.01, kulingana na hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa 2021/22, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema.
Amesema sambamba na hilo pia mapato yatokanayo na uwekezaji nayo yameongezeka na kufikia shilingi bilioni 745. “Hii haijawahi kutokea katika historia ya NSSF” amebainisha Mkurugenzi Mkuu wakati akitoa tathmini yake baada ya kupokea taarifa ya watendaji wa Mfuko walioshiriki kuhudumia wanachama na wananchi kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofikia kilele Julai 13, 2023.
Mshomba ametaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mara tu baada ya kuingia madarakani alikuja na mpango wa “Kuifungua Nchi” akilenga kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza nchini lakini pia kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania kupitia filamu ya “The Royal Tour”.
“Kichocheo kikubwa ni Mheshimiwa Rais alivyoweza kuwavuta wawekezaji, kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na waajiriwa, suala zima la uchangiaji limeongezeka, vipato vya wafanyakazi vimeongezeka na haya yote yamechangia kuongeza michango na kufanya kipato cha Mfuko kutokana na uwekezaji kuongezeka pia.” alifafanua Mshomba
Alisema sababu nyingine ni juhudi kubwa zilizowekwa na Mfuko katika kuboresha mifumo ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha utoaji wa huduma.
“Kulingana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unaishia Juni 2026, thamani ya Mfuko itafikia zaidi ya trilioni 11.5, na yote haya yanatokana na msukumo wa kuongeza waajiri na waajiriwa wanaochangia katika Mfuko lakini pia kazi nzuri inayofanywa na Mfuko.” alifafanua.
Kwa sasa thamani ya Mfuko wa NSSF ni trilioni 7.1, hivyo Mkurugenzi Mkuu amewahimiza Watanzania hususan kutoka sekta binafsi kujiunga kwa wingi ili kujenga maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Aidha, Mshomba amesema NSSF imepewa jukumu la kushughulika na sekta isiyo rasmi.
“Tunakamilisha taratibu za mwisho na tunaamini tukiweza kuwa na uchangiaji katika sekta isiyo rasmi, basi NSSF itazidi kupaa zaidi na kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hii.” alisema
Alisema idadi kubwa ya Watanzania wako katika sekta isiyo rasmi na wakiweza kujumuishwa kwenye mpango huo wa taifa litakuwa limefanikiwa kuondoa umaskini nchini.
“Kama ninavyosema siku zote hifadhi ya jamii iko kwa ajili ya kuwahudumia wananchama hasa kwa lengo la kuwaondolea umaskini pale wanapokoma kufanya kazi.” Alifafanua.
Kuhusu ushiriki wa NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Bw. Mshomba amesema wanachama zaidi ya 2,400 wametembelea na kuhudumiwa katika banda hilo kwa siku zote za Maonesho.
“Kumekuwa na mabadilio chanya ukilinganisha na mwaka jana, Wanachama wetu wamehudumiwa kwa kupatiwa elimu, usajili wa Wanachama, umuhimu wa kuwasilisha Michango kwa wakati na kuondoa kero mwanachama anapostaafu, elimu katika masuala ya uwekezaji, Mafao yatolewayo na Mfuko ambayo yanafikia saba lakini pia masuala ya Uwekezaji.” alifafanua.
Kuhusu Uwekezaji, Mshomba amesema wamebaini kuwa watu wengi wamevutiwa na eneo hilo.
“Kuna maeneo ambayo wanachama wetu wanaweza kufaidika moja kwa moja tunajenga nyumba na kuuza, au kupangisha kwa wateja.Hivyo aliendelea kwa kutoa rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za NSSF.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba ametembelea banda namba 13 la ushirikiano baina ya NSSF na PSSSF kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mfuko na kufurahishwa na huduma zote ambazo zilikuwa zinatolewa katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ‘Sabasaba’ yaliyofungwa na Mhe. Dkt. Husaein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tarehe 13 Julai2023, katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba akizungumza na mwanachama aliyetembelea katika banda la Mfuko, ambapo alimueleza kuwa pamoja na kuwa mwanachama wa sekta binafsi lakini bado anaweza kuchangia kwa hiari kupitia sekta isiyo rasmi kwa kuwa ina manufaa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, akizungumza jambo na mwanachama William Matee, aliyejiunga na huduma ya NSSF Taarifa Mobile App, ambapo sasa anaweza kutazama michango yake bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Matukio katika picha
Social Plugin