DK. NDUMBARO ATIMIZA AHADI YAKE, AKABIDHI MIFUKO YA SARUJI, KOMPYUTA


Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro amekabidhi mifuko ya saruji, kompyuta, pampu pamoja na tenki la maji kwa wakazi wa Matogoro, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Mhe. Dk. Ndumbaro amekabidhi vifaa hivyo vya ujenzi ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa alipotembelea shule ya Msingi Matogoro Julai 17 kukagua ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa.

Wakati wa ziara yake hiyo ya ukaguzi wa vyumba viwili vya madarasa, wananchi wa eneo hilo walimuomba Mhe. Mbunge huyo kuwasaidia saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyoo shuleni hapo pamoja na tanki la maji na pampu kwa ajili ya kisima walichoanza kuchimba wananchi hao.

“Leo ndugu zangu nimekuja kutekeleza yale mliyoniomba. Na kwa kujua pia umuhimu wa teknolojia, nimeamua kuwaletea kompyuta kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wetu pamoja na walimu kusoma kwa vitendo somo la kompyuta,” amesema Mhe. Dk. Ndumbaro.

Mhe.Ndumbaro pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa inayoendelea katika jimbo hilo katika sekta zote ikiwemo sekta ya afya na elimu.

“Mhe Rais ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vituo vya afya na shule. Tulikuwa tuna Kituo cha Afya kimoja ila kwa sasa tumeongeza saba. Mhe Rais pia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa ili watoto wetu wasibanane madarasani, hiyo ndio Serikali ya Awamu ya Sita na njia pekee ya kumlipa Mhe Rais Samia ni kuhakikisha tunamlinda na kumchagua tena,” amesema Mhe.Ndumbaro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post