Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

THBUB YAIOMBA SERIKALI NA WADAU KUANDAA PROGRAMU MAALUMU ZA KUWASAIDIA WANAWAKE.

 


Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawa Bora (THBUB) Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu), akitoa Tamko la Tume hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke wa Afrika Leo Julai 31, 2023 Jijini Dodoma.
Na Okuly Julius-Dodoma

Katika kuadhimisha siku ya Mwanamke wa Afrika ,Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora Imeiomba Serikali na wadau mbalimbali kuandaa programu maalum za kuwasaidia wanawake hasa wa vijijini kutumia teknolojia katika kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya usawa wa kijinsia.


Akizungumza na waandishi wa Habari leo Julai 31,2023 Jijini Dodoma,Mwenyekiti wa Tume hiyo Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu), akitoa Tamko la Tume hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke wa Afrika, ametoa wito kwa kwa wanawake kuendelea kujiamini na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.


"Siku hii muhimu pia inatukumbusha jukumu walilonalo wanawake wa kiafrika ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa ndani kama wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara, wanasayansi, na viongozi katika sekta nyingine nyingi,


Na kuongeza "katika kuadhimisha siku hii muhimu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaungana na jamii na wadau mbalimbali katika kutambua mchango wa Wanawake wa Afrika ambao walipigania kwa dhati ukombozi na maendeleo ya bara hili,"amesema Jaji Mstaafu Mwaimu


Aidha,Jaji Mstaafu Mwaimu amesema kuwa THBUB inaendelea kuwaenzi waanzilishi wa Umoja wa Wanawake wa Afrika kwa ushujaa wao, ambapo umechangia kuhamasisha haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika ajenda ya ukombozi wa Afrika.


"Viongozi wanawake, wengi tunaowaona leo kote barani Afrika, wanasimama juu ya mabega ya wanawake hawa jasiri, ambao walijitolea maisha yao kwa maendeleo ya Afrika,"amesema Jaji Mstaafu Mwaimu


Mwenyekiti hume amebainisha kuwa THBUB inaendelea kutambua na kuthamini jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa kipaumbele katika masuala ya kukuza usawa wa kijinsia na kuyaweka kuwa ni miongoni mwa ajenda muhimu za maendeleo za kitaifa na utekelezaji wake katika nyanja mbalimbali.


"THBUB inatambua pia kuwa Serikali imeweka msukumo mkubwa katika suala la kuhusisha masuala ya kijinsia katika sera, mikakati, programu za kisekta na kitaifa; uwezeshaji wanawake na kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia,"amesema Jaji Mstaafu Mwaimu


Tarehe 31 Julai ya kila mwaka ni maadhimisho ya Siku ya Mwanawake wa Afrika. Mwaka 1962 Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Barani Afrika iliazimia kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, na kutambua mchango wao mkubwa katika ukombozi na maendeleo ya Bara la Afrika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com