Na WMJJWM
Benki ya Dunia imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza jitihada za kuimarisha masuala ya jinsia katika jamii ikiwemo kuwainua wanawake kiuchumi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa masuala ya Jinsia wa Benki ya Dunia Hana Brixi wakati akizungumza na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima.
Hana amesema Mpango Mkakati wa Benki ya Dunia kuhusu maendeleo ya Jinsia kwa mwaka 2024 - 2030 unalenga maeneo muhimu ya ubunifu, rasilimali fedha na kuwezesha rasilimali watu ili kwa pamoja kutumia fursa za kiuchumi na kuhusisha wanawake katika uongozi katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Amebainisha kwamba Serikali ya Tanzania kupitia mradi wa PAMOJA unaofadhiliwa na Benki ya Dunia tayari inafanya jitihada hizo.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Dkt. Gwajima ameelezea juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia na kuimarisha usawa wa kijinsia nchini ni pamoja na kuundwa kwa madawati ya jinsia kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo na maeneo ya Umma.
Ameongeza pia uundwaji wa mabaraza ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ambayo ni sehemu ya kuwakutanisha wanawake na fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amebainisha afua mbalimbali zinazotekelezwa ikiwemo Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) hususani ujenzi wa vituo jumuishi vya kulea watoto ili kuwasaidia wanawake kufanya shughuli za kiuchumi.
Katika kikao hicho, kimehudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania Nathan Belete Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Badru Abdunur.
Social Plugin