NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Patrobas Katambi, amewataka Waajiri nchini kuwasilisha michango kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa wakati kama ambavyo Sheria inavyowataka kufanya hivyo.
Katambi ameyasema hayo Julai 6, 2023 alipotembelea banda la WCF kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa Sabasaba Katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Amesema Mfuko umekuwa ukifanya kazi nzuri sana katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo ni kulipa Fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
“Na kwa ndugu zangu waajiri niwaombe sana jitahidini kupeleka michango kabla hamjasukumwa na sheria, jitahidini kuwasilisha michango kwa wakati ili iweze kuwafaa wafanyakazi wenu. “Alisisitiza Katambi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma mpaka sasa Mfuko umeweza kusajili asilimia 90 ya waajiri wote nchini ambao wako kwenye kanzidata ya Mfuko.
“Tunaendelea kuwahimiza Waajiri waendelee kuwasilisha michango yao kwa wakati na Mfuko uendelee kulipa Mafao kadri ya wale wanaohitaji wanavyojitokeza.” Alifafanua.
Alitoa wito kwa wadau wa Mfuko ambao ni Waajiri waendelee kushirikiana na Mfuko kama inavyopasa lakini pia wadau wengine ambao ni wale wanaopata Mafao, amewahakikishia kuwa Mfuko wao uko imara na unaendelea kutoa Mafao kwa Mujibu wa Sheria.
Social Plugin