Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIASPORA WAOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA MBALIMBALI ZA UWEKEZAJI ZA NSSF, ZIKIWEMO ZA NYUMBA NA VIWANJA

 

 

Na MWANDISHI WETU

Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana, amewaomba Watanzania wanaoishi nje ya nchi  (Diaspora) kuona fursa ya kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na Mfuko kwenye maeneo mbalimbali nchini.


"Naomba Diaspora wote kuchangamkia miradi mbalimbali ya NSSF ikiwemo ya nyumba zilizopo Toangoma, Kijichi na Dungu jijini Dar es Salaam, pamoja na viwanja vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali ambavyo vinauzwa kwa gharama nafuu," amesema Balozi Bwana.

Amesema hayo tarehe 2 Julai, 2023 wakati alipotembelea banda la NSSF, ambapo ameweza kujionea namna wafanyakazi wa NSSF wanavyowahudumia kwa weledi wanachama na wananchi wanaotembelea banda hilo.

Balozi Bwana ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Diaspora wote kuitikia wito huo kwa kunufaika na fursa za uwekezaji kwa kununua nyumba na viwanja vya NSSF ambavyo ni vya uhakika.

Balozi Bwana amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni mdau muhimu wa NSSF, na kwamba wanashirikiana katika masuala mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na NSSF zinawafikia Watanzania wote wakiwemo wanaoishi nje ya nchi 'Diaspora'.

"Natumia fursa hii kuwapongeza NSSF wamekuwa na jukumu hili kwa muda mrefu wamekuwa na mifumo mbalimbali ya kutoa huduma za Hifadhi ya Jamii kwa Diaspora, lakini hivi sasa wanakamilisha mifumo mipya ambayo itaongeza ushiriki zaidi kwa Watanzania waliopo nje ya nchi," amesema Balozi Bwana.

Amesema pia Mfuko umekuwa ukiendesha miradi mbalimbali ya uwekezaji, na kwamba tayari wana ushirikiano wa karibu na NSSF ambapo hivi karibuni wana miradi mikubwa ya uwekezaji na uendelezaji inayofanyika nchini Kenya ili kuendeleza vitega uchumi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini nje ya nchi.

Balozi Bwana amesema uwekezaji wa NSSF hauishii tu katika uwekezaji wa ndani ya nchi, lakini sasa wanavuka mipaka na kwenda katika maeneo mengine nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kwenda kukusanya na kuleta faida zaidi kwa ajili kuwanufaisha wanachama wa NSSF.

"Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bwana Masha Mshomba, kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya ya kuhakikisha Mfuko unaendelea kusimama," amesema Balozi Bwana.

Aidha, ameipongeza Menejimenti na Bodi ya NSSF kwa kazi nzuri na miongozo ambayo wamekuwa wakiitoa katika kuhakikisha malengo makuu ya kuanzishwa kwa Mfuko yanaendelea kusimamiwa na kutekelezwa. Malengo hayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.

Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kulia kwa balozi ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele.

Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com