Na Mariam Kagenda _ Kagera
Serikali mkoani Kagera imesema itaendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaohatarisha uhuru na usalama wa Taifa sambamba na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanaoshiriki kuandikisha na kuwapa nyaraka mbalimbali za uraia watu ambao sio watanzania.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Mh.Fatma Mwassa amesema hayo wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya mashujaa iliyotanguliwa na sala ya kuwaombea mashujaa na kutembelea makaburi ya mashujaa hao waliopigana vita vya Kagera mwaka 1978_1979 ambapo maadhimisho hayo yamefanyika katika kambi ya Kaboya kikosi cha 21 JWTZ wilaya ya Muleba.
Mhe. Mwassa amesema kuwa wameisha baini baadhi na wataendelea kuchukua hatua kwani wale wote wanaowaandikisha watu ambao sio watanzania na kuwapa hati za kuonyesha kwamba ni Watanzania ilihali wanajua sio Watanzania ni raia wa nchi nyingine hawatohamishiwa vituo vingine vya kazi bali watafukuzwa.
Ameongeza kuwa kuna kila sababu na wajibu wa kulinda mipaka kwasababu Kagera ni mkoa ambao uko mpakani na umepakana na nchi nyingi na kuna mashujaa ambao walifariki kwa kupigania uhuru hivyo serikali haitokubali kuona mtu anachezea amani na anahatarisha usalama wa nchi ya Tanzania.
Amewahimiza wananchi kuendelea kuwaenzi mashujaa hao kwa vitendo na kulinda rasilimali za nchi ya Tanzania na kuwa wazalendo kama ilivyokuwa kwa mashujaa waliojitoa kwa ajili ya nchi yao.
Kwa upande wake askari mstaafu wa Jeshi la wananchi wa Tanzania aliyepigana vita vya Kagera Haidari Issa amesema kuwa moja ya sababu ambayo ilipelekea kushinda vita ni umoja na mshikamano waliokuwa nao licha ya kuwa walikuwa wanapitia wakati mgumu.
Social Plugin