Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo amewataka viongozi wa CCM kutokujibu matusi yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani juu ya suala la uwekezaji wa bandari bali wajikite katika kutekeleleza miradi ya maendeleo ili kuwajibu kwa vitendo.
Chongolo ameyasema hayo wakati wa mkutano wa Mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa uliofanyika Julai 30,2023 uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza .
Amesema msimamo wa CCM ni kuongeza kasi katika utekelezaji wa ilani ya CCM na kama chama hawapo tayari kupoteza muda kwa ajili ya kujibu matusi yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwani suala la ukosoaji limekuwa likijitokeza tokea kipindi cha nyuma na tayari ukosoaji huo wameuzoea.
"Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero za wananchi,ukosojai huu haujaanza leo hivyo Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wananchi kwa kuwaletea maendeleo”,amesema Chongolo.
Aidha Chongolo pia amesema wanaopinga mkataba huo wanataka kukichonganisha Chama Cha Mapinduzi na wananchi wake ili kishindwe kutekeleza ilani ya chama hicho na wao watumie fulsa hiyo kuwadanganya wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela, ambae pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula, amesema suala la uwekezaji bandari ni ufunguo wa uchumi wa Taifa hivyo wananchi wanatakiwa kuungana kwa kauli moja ili suala la uwekezaji katika bandari liweze kuidhinishwa.
“Suala la uwekezaji wa bandari ni ufunguo wa taifa letu kiuchumi,wale ambao hawajelewa tutasubiri ufahamu wao ufunguke,”ameeleza Dkt. Angeline.
Sanjari na hayo amefafanua kuwa Sheria ya Ardhi Namba 4 inabainisha namna bora ya kumilikisha ardhi kwa wawekezaji,watapewa hati ya muda wa kupanga katika ardhi hiyo si kuwamilikisha jumla.
Pia amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, shughuli za maendeleo hazijasimama mkoani Mwanza na Jimbo la Ilemela ambapo Trilioni 4.556 zimetolewa kwa miradi ya kimkakati na kuimarisha huduma za jamii.
Akichangia hoja katika mkutano huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema, kwa nchi ya Tanzania sehemu ya bandari ndiyo inayoongoza kwa kuingiza shehena kubwa ya mizigo inayotoka sehemu mbalimbali hivyo bandari ya Dar es Salaam ikiboreshwa itasaidia kuingiza na utoa mizigo kutoka nchi mbalimbali na hii itasaidia katika kukuza uchumi wa taifa.
Pia ametoa ufafanuzi kwa wananchi kuwa uwekezaji wa bandari ya Dar-es-Saalam utahusisha kupangishwa kwa magati matano na siyo kuuzwa kama inavyodaiwa na wapotoshaji.
Amesema mwaka wa fedha ulioisha mapato ya bandari zote nchini yanayosimamia na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) yalikuwa bilioni 795.2 na kutumia zaidi ya bilioni 791 huku TRA ikikusanya trilioni 7.76 katika bandari ya Dar es Saalam, hivyo upitia uboreshajina uwekezaji wa bandari makusanyo ya TRA yataongezeka mpaka trilioni 26.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando amesema Oktoba 25, 2022 serikali iliingia mkataba wa makubaliano ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha shughuli za bandari mkataba ambao baada ya kusainiwa uliridhiwa na Bunge.
“TPA haijauza bandari na hakuna mwekezaji ameuziwa ardhi ya bandari, masuala yote ya ardhi yatasimamaiwa kwa mujibu wa sheria halali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Sheria namba 4 ya Ardhi imeweka wazi, waache uongo hakuna bandari imeuzwa,”amesema Wakili Msando.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula,amesema kwa bajeti ya trilioni 44.3, bado taifa linahitaji kupata vyanzo vingi vya mapato hili bajeti hiyo ilifikie asilimia 100 na kuwezesha miradi ya kijamii itekelezwe kwa ufanisi hivyo uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam unahitajika.
NaYe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla,kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya amemshukuru Rais Samia kuleta fedha katika Mkoa huo kiasi cha trilioni 1.4 za miradi ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati huku akiridhia kutoa bilioni 130 za kuiwezesha Wilaya ya Ukerewe kupata umeme wa uhakika.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni Daraja la Kigongo-Busisi ambao umefikia asilimia zaidi ya 75, SGR kipande cha Mwanza-Isaka kinachojengwa kwa trilioni 3 umefikia asilimia 32, Meli ya MV Mwanza iliyogharimu bilioni 108 umefikia asilimia 95 huku ukarabati wa meli ya mizigo ya MV.Umoja ukigharimu bilioni 20.
“Yanayoendelea ya uwekezaji wa bandari ni wivu wa maendeleo na siasa ambapo siasa hujibiwa kwa siasa,uongo ukiachwa unakuwa ukweli,hivyo wananchi wa Kanda ya Ziwa wanaunga mkono uwekezaji huo kwani watakuwa wanufaika wakubwa kupitia bandari Kavu Fella,meli ya Umoja na daraja la Kigongo-Busisi, zitapokea mizigo na kuisafirisha kwenda nchi jirani,”.
CCM kupitia Katibu Mkuu wake Daniel Chongolo wamehitimisha mkutano wa hadhara maalumu kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuhusu mkataba wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari katika Mkoa wa Mwanza baada ya kufanya mikutano mingine 7 ikiwemo Mbeya, Mtwara,Arusha,Tanga,Singida, Kigoma,Dar-es-Salaam.
Social Plugin