Tume ya Tehama nchini (ICTC) imetangaza kuanza kwa maandalizi ya Kongamano kubwa la Mwaka la Tehama kwa Mwaka 2023 litakalowakutanisha wadau kutoka Sekta mbalimbali Tanzania kujadili mwenendo wa TEHAMA nchini na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha huduma za Tehama nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt.Mwasaga Nkundwe amesema kuwa kongamano hilo litafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 16 hadi 20 Oktoba, 2023.
"Kongamano hili litajikita hasa katika kuangalia mabadiliko ya kidijitali nchini kuelekea kukua kwa Teknolojia mpya ulimwenguni, tutajikita hasa katika kuangalia matumizi ya akili bandia katika uchumi wa kidijitali (Artificial Intelligence)," amesema.
Amesema kwa mwaka huu wanatarajia wadau zaidi ya 5000 watashiriki ikilinganishwa na wadau 2500 kwa mwaka uliopita waliotoka ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amezindua kadi za kieletrokini kwa washiriki wote na watapata huduma zote za TEHAMA.
"Niwaombe wadau wote wa TEHAMA ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi katika kongamanano hili la Saba la Tehama nchini kujionea huduma na bunifu mbalimbali za Tehama pamoja na kubadilishana ujuzi baina ya washiriki,"amesema.
Social Plugin