Na
Mwandishi wetu _ Same
Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), kwa kushirikiana na ofisi ya
mkuu wa Wilaya Same imetoa elimu kwa wananchi wa kata ya Tae wilayani Same
mkoani Kilimanaro kuhusu madhara ya kujihusisha na kilimo, biashara na matumizi
ya dawa za kulevya aina ya mirungi ikiwa ni siku chache baada ya operesheni
tokomeza mirungi iliyofanyika katika kata hiyo na kufanikisha uteketezai wa
hekeri 535 za mashamba ya Mirungi na kukamatwa kwa watuhumiwa 9. Elimu hiyo
imetolewa tarehe 12 Julai, 2023 katika kikao maalumu kilichowahusisha maafisa
wa DCEA, viongozi wa wilaya ya Same, wataalamu ya masuala ya kilimo na bishara pamoja
na wakazi wa kata hiyo.
Akizungumzia athari za
matumizi ya mirungi, Kamishna wa Kinga na Tiba DCEA, Dkt. Peter Mfisi ameeleza kuwa matumizi ya mirungi yanachochea uhalifu ikiwemo ugomvi na mauaji kwa sababu ya kuathiri uwezo wa kufikiri, jambo linalosababisha mtu kuchukua maamuzi yoyote pasipo kutafakari matokeo yake na kusema kuwa baadhi ya maeneo ambayo kilimo cha mirungi yamekithiri kuna changamoto kubwa wananchi wake kitabia.
“Watoto wenu wakianza kutafuna mirungi mtazalisha
kizazi chenye migogoro na mafarano yasiyo isha. Watu mtashindwa kutatua hata
changamoto dogo ndogo zinazowataka mkae chini na kuzijadili badala yake
mnachukua mapanga na mikuki na kuanza kushambuliana” amesema Dkt. Mfisi.
Afisa kilimo wa halmashauri ya Same Bw. Mohammed
Muhina ameyataja baadhi ya mazao ya biashara yanayostawi katika maeneo hayo
yayoweza kuwa mbadala wa kilimo cha Mirungi.
“Eneo la Same linakubali mazao mbalimbali kama
tangawizi, zao la vannila ambalo tayari limeanza kulimwa katika baadhi ya maeneo,
lakini pia kuna zao la kahawa na mazao mengine mengi kama migomba na kadhalika”
amesema Muhina.
Nae Kamishna wa Huduma za Kitengo
cha Sheria DCEA, Veronica
Matikila amesema Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Na. 5 ya
Mwaka 2015 inakataza kilimo, kuhifadhi na ukusanya
wa mazao haramu ikiwemo mirungi na bangi na adhabu yake ni kifungo cha miaka
thelathini (30) jela au kifungo cha maisha.
Hivyo, yoyote
anayejishughulisha kwa namna yoyote na dawa za kulevya anatenda
kosa na akibainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo
ametoa rai kwa viongozi
wa halmashauri kuanzia maafisa tarafa na wenyeviti wa vitongoji kuwajibika kuhakikisha wanadhibiti
uhalifu wa kilimo na matumizi ya mirungi, pamoja na kutoa elimu kuhusu athari
ya matumizi yake katika maeneo wanayosimamia kulingana na sheria za nchi.
"Ni wajibu wa kila
kiongozi katika halmashauri kuhakikisha anadhibiti matumizi ya mirungi, ikiwa
ni pamoja na kukomesha kilimo chake kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu
shughuli mbadala wanazoweza kuzifanya ikiwemo kilimo cha mazao mengine yenye
tija. Pia, kuwatumia wataalamu wa halmashauri kutoa ujuzi
kwa wananchi utakaowasaidia kwa
namna moja au nyingine kufanya biashara halali zitazokuwa chanzo cha mapato kwa
ajili ya kujikimu na maisha na kuachana na biashara ya
mirungi." amesisitiza Kamishna Jenarali Lyimo.
Katika hatua nyingine,
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni aliagiza viongozi wa kata ya Tae kuhakikisha
ndani ya mwezi mmoja visiki vyote ving’olewe na mashamba yote ambayo hayakufikiwa wakati
wa operesheni yateketezwe, ambapo utekelezaji wake umeanza tarehe 12 Julai,
2023 ukiongozwa na afisa mtendani wa kata ya Likweni Isaack Stephano Mwansasu.
Vilevile, mkazi wa kata ya Tae, Elisante
Semkondo amesema asilimia kubwa ya vijana katika kata hiyo wanatumia mirungi kutokana na
tabia ya kuiga. Hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuwapa elimu kuhusu mirungi na dawa za kulevya
kwa ujumla kwa kuwa itaongeza hamasa kuchukua hatua ya kudhibiti changamoto hiyo na
kuachana kabisa na kilimo cha mirungi.
Operesheni hiyo ya kutekeza
mirungi katika mkoa wa Kilimanjaro ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha
inadhibiti na kutokomeza matumizi ya dawa ya kulevya
na imekuja ikiwa wiki
kadhaa tangu kufanyika Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan aliagiza kufanyika
kwa operesheni endelevu ikiwa
ni pamoja na viongozi wote wa Serikali kushiriki katika kupambana na dawa za
kulevya katika maeneo yao.
Katika kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais, Mkuu wa wilaya ya
Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda akishirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na
kupambana na dawa za kulevya jana tarehe 13 JulaI, 2023 ameviongoza Vyombo vya Ulinzi na
Usalama wilayani humo
katika operesheni maalumu katika kijiji cha Kisimiri na kufanikiwa kuteketeza
gunia 280 na mbegu kilogramu 300 za bangi na kukamatwa
kwa watuhumiwa 4 wakihusishwa na bangi
hizo.
Social Plugin