NA MASHAKA MHANDO Mkinga
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga Ustadh Rajab Abrahaman Abdalah amesikitishwa na usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo unaofanywa na halmashauri ya wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Mwenyekiti alizungumza hayo jana wakati akikagua kwa nyakati tofauti, ujenzi wa zahanati za vijiji vya Mzingi-Mwagogo iliopo kata ya Parungu-Kasera, zahanati ya kijiji cha Temboni kilichopo kata ya Maramba na shule ya msingi Mwandusi- Mtundani iliopo kata ya Manza.
Akikagua ujenzi wa zahanati ya Mzingi-Mwagogo, ambayo imepakwa rangi kabla ya ujenzi wake kukamilika ikiwa imetumia hadi sasa shilingi milioni 67, alisema miradi hiyo kumekosekana nguvu ya usimamizi na kufanyika matumizi mabaya ya fedha.
Alisema ilani ya CCM inaelekeza kila kijiji kiwe na zahanati lakini viongozi hao kwa miaka kumi wameshindwa kuwaondolea wananchi kero ilidumu miaka mingi na kusababisha akina mama wajawazito kujifungulia njiani wakifuata huduma Vijiji vya jirani.
"Kila aliyepewa dhamana na serikali lazima atimize wajibu wake, msipofanya haya mnakifanya Chama Cha Mapinduzi kipate wakati mgumu inapofika uchaguzi wakati fedha zinaletwa lakini viongozi wanashindwa kuzisimamia, kiukweli chama hakijaridhika na kimesikitishwa na uzembe wa viongozi kushindwa kusimamia fedha hizi," alisema Mwenyekiti.
Mwenyekiti alisema uwamuzi uliotumika kupaka rangi jengo hilo haukuwa sahihi kwasababu huwezi kupaka mafuta kabla ya kuoga ambapo wangetumia fedha hizo kununua milango na madirisha jengo hilo lingeweza kutumika kwa muda mfupi na kuwasaidia wananchi hao.
Halkadhalika pia alikuta matumizi mabaya ya fedha kwenye zahanati ya Matemboni ambayo hadi sasa tayari imetumia kiasi cha shilingi milioni 62 wakibakisha milioni 3 ambazo haziwezi kumaliza ujenzi huo ambao hadi sasa wanajenga zahanati hiyo kwa miaka kumi sasa.
Pia alipofika katika ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya msingi Mwandusi-Mtundani alikuta madarasa mawili yamejengwa chini ya kiwango licha ya serikali kuleta fedha nyingi.
Mwenyekiti alisema haikubaliki majengo hayo kujengwa chini ya kiwango ilhali viongozi wapo wanashindwa kusimamia fedha hizo wakati Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akileta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya huduma za jamii.
Kufuatia hatua Mwenyekiti huyo alitoa maelekezo maelekezo kwa mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali (Mstaafu) Maulid Sulumbu afuatilie miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati ili kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu.
Lakini pia amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha watu waliochezea fedha katika miradi hiyo wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine na Mwenyekiti aliahidi kurudi tena wilayani humo kuona kama miradi hiyo imekamilika na kuanza kazi.
Mbunge wa jimbo hilo Dastan Kitandula alimpa Mwenyekiti huyo salamu za Rais Dkt Samia kwamba wameridhika na kazi anazozifanya hasa kuwaletea fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo suala la maji.
Wananchi mbalimbali waliozungumza na blog hii, wameonesha kurodhishwa na ziara ya Mwenyekiti kupitia na kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya CCM.
"Hatujawahi kuwa na Mwenyekiti anayekuja wilayani na kulala huko kwa siku nne, kiukweli kura zetu hazikupotea bure, tunaye Mwenyekiti mwenye uwezo na utashi wa kusimamia kazi za chama.
Social Plugin