MAFUNZO YA WALIMU KAZINI KUWA ENDELEVU - PROF. MKENDA



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Pof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata yanayotolewa na Wizara hiyo jijini Mwanza.

Na.Mwandishi Wetu-MWANZA

SERIKALI imesema itawekeza katika elimu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mafunzo ya walimu kazini yanakuwa endelevu kama inavyoelekezwa katika Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 Toleo la 2023 inayotaka walimu wote waliopo kazini kuendelezwa kupitia vituo vya walimu (TRCs) pamoja na kuwawezesha watakaopenda kujiendeleza.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Pof. Adolf Mkenda Jijini Mwanza wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata yanayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema serikali itawekeza kwa walimu waliopo kazini na kulinda ajira zao na kwamba vituo vya walimu (TRCs) ambavyo vitasimamiwa na Maafisa Elimu Kata vitakuwa chachu ya kuendeleza walimu sasa kuliko wakati wowote.

Prof. Mkenda amesema mafunzo yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Halmashauri zote kwa walimu wa ngazi mbalimbali na viongozi wasimamizi wa elimu nchini ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo na kwamba mafunzo hayo yatakuwa endelevu hasa kwa walimu wa sayansi na Hesabu.

“kinachofanyika leo hapa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa maelekezo ya kuhakikisha tunaendeleza mafunzo ya walimu kazini pamoja na ya matumizi sahihi ya vishikwambi. Tayari Katibu Mkuu ameshapanga timu ya kutoa mafunzo hayo nami pia nimekuja hapa kushuhudia ” amesema Prof. Adolf Mkenda

Kiongozi huyo ameongeza kuwa nchi zinatofautiana katika maendeleo na hasa ni kutokana na elimu na uwekezaji kwenye sayansi na teknolojia na si utajiri wa rasilimali na ndio maana watu wanalinganisha Korea na Tanzania kwamba miaka ya 1961 hazikuwa zikitofautiana sana kiuchumi lakini sasa Korea ni nchi ya uchumi wa Juu ni sababu wamewekeza katika Elimu.

“Nchi za Scandinavia zimeendelea zikiwa hazina rasilimia nyingi za asili lakini kutokana na jinsi walivyowekeza katika elimu na wakatumia elimu kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu ambavyo vimewasaidia kuanzisha bidhaa nyingi ambazo zinashindana katika soko la dunia ikiwemo utengenezaji wa magari, simu na kuwawezesha watu wao kutumia vyema rasilimali zao ndogo za asili kwa maendeleo ya mataifa yao” amesisitiza Prof. Mkenda.

Amesema ili kujenga nchi yenye maendeleo kwa vizazi na vizazi njia kubwa na pekee ni kuwekeza sana kwenye elimu amewaataka Maafisa elimu kata kufahamu kuwa wao ndio wasimamizi wakubwa katika elimu huku akiwataka kutambua kuwa wanasimamia kitu muhimu kwa ajili ya kizazi cha leo na kijacho.

“Na ndio maana Mimi nasema Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoweka kipaumbele katika elimu, kwa uwekezaji na kwa mageuzi makubwa tunaendelea nayo katika Sekta hakika tumpe maua yake na atakumbukwa daima. Mafunzo kwa walimu kazini ni sehemu ya uwekezaji huo, kuna tabia ya watu kubeza wasomi na kudharau elimu tuwe waangalifu sana kwani bila elimu hatuwezi kuwa na madaktari, wahandisi na wengine” ameongeza Waziri huo.

Amesema kuwekeza kwenye mageuzi ya elimu matunda yake hayaonekani mapema kuna kazi kubwa itafanyika mpaka yaanze kuonekana kwani utekelezaji wa mageuzi hayo utakwenda kwa awamu ili elimu isivurugwe.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na TEknolojia Prof. James Mdoe amesema kuna matarajio makubwa kutoka kwa Maafisa Elimu Kata hao na kwamba watakwenda kutekeleza kazi kwa bidii kwani serikali inataka kuona mabadiliko katika elimu kwa sababu wao ndio viongozi wa elimu walio katika ngazi za chini.

“Matarajio yetu ni kuona ninyi nakwenda kusimamia vituo vya walimu kwa weledi na kuhakikisha mafunzo ya walimu yanatolewa na vituo hivyo vinatumika ipasavyo, sisi tunataka kuona mabadiliko katika ufundishaji na ujifunzaji baada ya mafunzo haya” amesisitiza Prof Mdoe

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Huruma Mageni amesema kuwa Maafisa Elimu Kata wana jukumu la kuendesha na kusimamia Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA) katika ngazi ya shule na vituo vya walimu, hivyo kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeandaa mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata 2,384 nchini kuhusu uendeshaji na usimamizi wa MEWAKA

Ameongeza kuwa baada ya mafunzo hayo kukamilika jumla ya walimu 45,979 na viongozi wa Elimu 3,412 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Maafisa Elimu Kata 2,730 kutoka Halmashauri 184 watakuwa wamejengewa uwezo wa kuendesha na kusimamia MEWAKA katika Shule na Vituo vya Walimu.






Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Pof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata yanayotolewa na Wizara hiyo jijini Mwanza.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na TEknolojia Prof. James Mdoe,akizungumza wakati wa Mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata yanayotolewa na Wizara hiyo jijini Mwanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post