MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Jumanne Mtaturu Julai 5,2023, amechangia ujenzi wa Ofisi ya CCM Wilaya ya Ikungi ili kusaidia kukamilisha ujenzi huo.
Bingwa huyo wa siasa za "Maneno kidogo, kazi zaidi," amekabidhi Mifuko 50 ya saruji, Mbao za kufanyia blundering na kokoto lori 3 vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 3.9.
Akikabidhi kwa niaba ya mbunge, Ally Rehani ambaye ndiye katibu wa mbunge huyo, amesema amepeleka vifaa hivyo ikiwa ni muendelezo wake wa kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM wilaya ambayo ndani yake kuna ukumbi mkubwa wa mikutano.
"Kukamilika kwa Ukumbi huu itakifanya chama kuwa na uhakika wa vikao vyake sehemu salama na yenye hadhi" alisema Rehani.
Akipokea vifaa hivyo katibu wa CCM wilaya Stahmili Dendego amemshukuru Mbunge Mtaturu kwa moyo wake wa kukisaidia chama kila mara.
Ameeleza mchango wa leo ni miongoni mwa michango mingi aliyokipatia chama.
Sio mara ya kwanza kwa Mtaturu kuchangia ujenzi huo ambapo Mei 8,2023,alikabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh.Milioni 1.8 ambavyo ni Gypsum Board 75 na ndoo tano za rangi ambavyo alivikabidhi mbele ya Kamati ya Siasa ya Wilaya.
Mbali na kutoa msaada wa kifedha,Juni 15,2021,Mtaturu pia alichangia nguvu kazi kwa kushiriki uzinduzi wa ujenzi wa ofisi hiyo ambapo kwa kushirikiana na viongozi wa CCM Wilaya na Wananchi walichimba msingi wa jengo hilo.
Aidha,katika uzinduzi huo alichangia bati 100 na mifuko ya saruji 100 vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 5.9.
Social Plugin