Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE SEKIBOKO ATEMBELEA VIKUNDI VYA WAKINA MAMA VILIVYONUFAIKA NA ASILIMIA 10 YA MAPATO YA JIJI LA TANGA

 

Mbunge Husna Sekiboko (kishoto) akizungumza katika mkutano wa Mabokweni alipotembelea chanzo cha maji. Akiwa na Mwenyekiti wa UWT Jiji la Tanga Moza Shilingi

 NA MASHAKA MHANDO, Tanga


MBUNGE wa viti maalumu mkoani Tanga, Husna Sekiboko, ametembelea vikundi vya akina mama vilivyokopeshwa fedha kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga.


Mbunge huyo ambaye amekuwa karibu na Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Tanga kutokana na kufanya kazi kwa pamoja na Jumuiya hiyo, alitembelea vikundi vya ufugaji kuku, usagaji nafaka pamoja na uuzaji wa unga wa chakula.


Akizungumza na akina mama hao katika kikao kilichofanyika kata ya Mnyanjani na kisha mkutano kule Mabokweni ambako alizungumza na wananchi wa kata za  Nguvumali na Chumbageni, alisema mikopo waliyopewa vikundi hivyo vya ujasirimali watumie pesa hizo kujenga uchumi wao na kupiga hatua.


Alisema fedha walizopewa zinatakiwa zirejeshwe ili ziweze kukopesha wajasirimali wengine kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwasaidia ili waweze kuinuka kiuchumi.


Hata hivyo, alisema mikopo hiyo inayotolewa na serikali asilimia nne vijana na wanawake na asilimia mbili makundi ya watu Wenye ulemavu, kwasasa imesitishwa ili kuboresha kwa makundi hayo tofauti na awali.


Mbunge huyo aliipongeza halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kuweza kutoa fedha nyingi za mikopo tofauti na wilaya nyingine alizopita baada ya kukuta kikundi kimoja kimepewa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 40.


"Kiukweli nimetembea wilaya nyingine na hata kule kwetu Lushoto hakuna mjasiriliamali ambaye halmashauri imeweza kumkopesha fedha kama hizi sana sana huko wanawakopeshwa shilingi milioni mbili au tatu," alisema mbunge.


Alisema fedha hizo wasione zinatolewa tu kwa bahati mbaya bali  ni usimamizi mzuri wa mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya.


"Muungeni mkono mbunge wenu (Ummy) ni kiongozi makini na ndiyo maana ameaminiwa na kupewa uongozi, mnaweza msione umuhimu wake lakini nawaambia mshikeni sana mbunge wenu," alisema Sekiboko.


Mbunge huyo alisema kuwa ziara yake katika jimbo la Tanga, ni kukutana na wanachi kujua changamoto zao lakini pia kuwaomba wananchi wamuunge mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri anayoifanya nchini ikiwemo mkoa wa Tanga.


Alisema akina mama wanao wajibu mkubwa wa kumuunga mkono Rais licha ya kuwa mwanamke mwenzao lakini ametekeleza miradi mingi ya maendeleo nchini katika sekta za afya, elimu, maji na miundo mbinu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com