MIAKA 60 YA JKT YAADHIMISHWA KWA KISHINDO





Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameshiriki sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT)huku akiielekeza Wizara ya Ulinzi na JKT kuandaa mpango mkakati wa kurekebisha makambi kwenye Jeshi la JKT katika upande wa malezi ya vijana.

Akizungumza leo Julai 10,2023 jijini hapa kwenye maadhimisho hayo Rais Samia ameitaka pia Wizara hiyo, kuliwezesha Shirika la SUMA JKT kupata mikopo ili wazalishe na waweze kurejesha mikopo na shirika liweze kuendelea, na kwamba kama ikitakiwa udhamini wa Serikali itakuwa tayari.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuiboresha JKT ili liwe Jeshi la kisasa zaidi linaloendana na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu, mafunzo yanayotolewa na JKT yawasaidie vijana kuwa wazalendo wa kweli wanaothamini utaifa, umoja na mshikamano wa Watanzania na wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea.

"Kwa vijana watakaoendelea na kazi katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama baada ya  mafunzo yao, nataka wawe na weledi wa kuaminika, kutumainiwa na wanaoweza kweli kuilinda na kuitetea nchi yao bila hofu,"amesema 

Rais Samia amesema JKT ilianzishwa rasmi Julai 10, 1963, ambapo hatua hii ilikuwa ni utekelezaji wa azimio la kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Aprili 19, 1963 chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwl. Julius Nyerere.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema mafunzo ya JKT ni sehemu muhimu ya mchango wa amani iliyopo nchini na kwamba Wizara itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta kuboresha mafunzo stadi za kazi kwa vijana wa JKT na kuwawezesha kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ya ilivyo sasa ili baada ya kuhitimu mafunzo hayo waweze kujitegemea na kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali bila kusahau maendeleo ya michezo na sanaa.

Amesema ili kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Wizara yake itashirikiana na sekta za kilimo, mifugo na uchumi wa buluu pamoja na kufungamanisha sekta hizi na sekta ya viwanda ili kuimarisha JKT na JKU kuwa vyombo vya kuwapatia vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa, pia kuwa vyombo mahiri vya huduma za uzalishaji mali.

"Dhumuni kuu la kusanyiko hili ni  kikubwa kubadilisha fikra za kikoloni kwa vijana waliohudhuria mafunzo yake, JKT imefanikiwa kuwajenga vijana katika hali ya umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu, uelewano bila kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini, jinsia hivyo kudumisha uhuru na amani ya Taifa letu,"amesema 

Akitoa taarifa ya JKT Meja jenerali Rajabu Mabele amesema Jeshi hilo Lina majukumu ya uzalishaji mali na ulinzi wa Vijana na kwanza limefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia katika Jeshi hilo. 

Amesema ni mahali ambapo vijana wa itikadi zote, rangi zote, makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja.

"JKT limekuwa mfano wa malezi ya vijana  pengine hata ile tabia ya Watanzania wengi kutoulizana mabila imetokana na kuwa na vijana wazalendo wa wanaopitia JKT,huwa wanakutana na vijana mbalimbali kutoka kila kona ya nchi yetu, ndiyo maana hawana muda hata wa kuulizana makabila kwa vile wote hujiona ni wamoja,"amesema.

Amesema majukumu ya msingi ya JKT ni malezi ya vijana, uzalishaji mali na ulinzi wa Taifa, tangu kuanzishwa kwake rasmi Julai 10, 1963, hadi sasa Jeshi hili linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

"JKT imefanikiwa kuwa na ongezeko la idadi ya vijana wanaopata mafunzo ya Jeshi hili ambapo mwanzo lilianza na vijana 11 lakini kwa sasa vijana waliopo makambini wanaohudhuria mafunzo kwa mujibu wa Sheria ni 52,000,"amesema 

Amesema Uanzishwaji wa vikosi, kambi mpya za JKT na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya vikosi, umesaidia kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki mafunzo ya JKT. JKT imekuwa ni chombo muhimu cha muwajenga vijana na kukuza uzalendo

Pamoja na hayo alisema JKT inaendelea kuaminika na kufanya miradi muhimu ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino pamoja na majengo na miradi mingine ya Serikali. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post