MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amegawa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 16.6 na kuzindua rasmi Mashindano ya East Singida Inter School Sports 2023,yanayohusisha shule 19 za serikali na binafsi zilizopo Jimboni humo.
Akigawa vifaa na kuzindua mashindano hayo Julai 14,2023,katika viwanja vya shule ya sekondari Ikungi ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Rashid Mohammed Rashid,Mbunge Mtaturu amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji shuleni na kuwaandaa vijana kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Amesema vifaa alivyogawa ni seti 38 za michezo zenye gharama ya Sh Milioni 10.6 na mipira 120 yenye thamani ya Sh Milioni 6.
“Hatua hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM na kuunga mkono kwa vitendo jitihada za serikali yetu za kuinua soka nchini tukikuza vipaji hivi mapema tutakuwa na vijana watakaoiokoa nchi kwenye tasnia ya michezo,mimi niwahakikishie kuwa nitaendelea na jitihada zangu hizi kila mwaka,”amesema.
Akitaja zawadi za washindi wa mashindano hayo Mtaturu amesema ili kuweka chachu kwa wachezaji wamekubaliana zawadi ya mshindi wa tatu iwe mashine ya uchapishaji moja na mpira,mshindi wa pili atapata kompyuta na mipira miwili na wakwanza atapata mashine ya uchapaji moja,kompyuta moja na mipira mitatu ambazo zitatolewa kwa washindi wa mpira wa miguu na mpira wa pete.
“Kama kamati tuliona tuweke chachu zaidi katika mashindano haya,tukasema safari hii tutoe vifaa vitakavyochochea uboreshaji wa elimu,tulikaa tukasema kwa sababu shul ni kubwa tukitoa Sh Milioni moja watu watagawana kidogo kidogo haitokidhi mahitaji,tukisema tuchinje mbuzi au ng’ombe atachinjwa ataliwa siku moja halafu basi,ndio maana tukaona tuboreshe zaidi,”amesema.
Amesema zawadi hizo pia zitaenda kwa mfungaji bora,mchezaji mwenye nidhamu,mchezaji bora,mdakaji bora kwa upande wa mpira wa miguu ambao kila mmoja atapata Sh 50,000.
“Niwaombe tucheze kwa nidhamu,sisi tunataka mcheze kwa haki msiumizane kwa kuwa michezo ni furaha,”amesema.
Social Plugin