NDEGE MPYA YA MIZIGO YA TANZANIA YAANZA SAFARI


Kampuni ya Ndege Air Tanzania (ATCL) leo imeanza safari yake ya kwanza ya ratiba ya kusafirisha mizigo kwa kutumia Ndege yake ya mizigo Boeing 767-300F iliyowasili nchini mapema mwezi Juni 2023.

Hayo ameyasema leo Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo bwana Patrick Ndekena wakati akiongea na waandishi wa habari, katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salam.

Mkurugenzi huyo amesema ratiba ya safari za Dubai itakuwa mara mbili kwa wiki ambapo jukumu la ATCL kwa ndege hii ni kuhakikisha bidhaa za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi zinafika kwa wakati na zikiwa na ubora wake kwenye nchi mbalimbali kwa kadri ya mahitaji.

“Leo tunafuraha kubwa kwa kuanza rasmi safari zetu za ratiba kwa ndege yetu hii mpya ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kusafiri masafa marefu na uzito mkubwa yaani tani 54 kwa mara moja, kwa Dubai peke yake tutakuwa na safari mbili kwa wiki, Jumatatu na Ijumaa”.

Akifafanua kuhusu uwezo wa ndege hiyo, amesema Boeing 767-300F ni ndege ya kisasa yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 850 kwa saa na kukaa angani kwa zaidi ya masaa 10 bila kutua.

Kuhusu wataalamu wa ndege hiyo ameeleza kuwa ATCL ina marubani wakitanzania sita (6) waliobobea kwenye ndege hii. Wataalam wengine wabobezi ni pamoja na wahandisi wa ndege ambao pia ni watanzania.

Ndekana amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha ATCL kujiendesha kibiashara.

Naye wakala wa usafirishaji mizigo Bw. George Magoti amesema uwepo wa ndege hii ni mkombozi kwa wafanyabiashara nchini kwani itawasaidia kupunguza gharama za usafirishaji. Magoti amefafanua kutokana na ukubwa wa mizigo hii, isingewezekana kusafirishwa kwa ndege ya abiria hivyo wangelezimika kukodi ndege ya mizigo kutoka nje ya Tanzania ili kuweza kupakia mizigo mikubwa ya aina hii.

“Tunashukuru ATCL kukubali kufanyabiashara nasi ya mizigo la sivyo tungelazimika kutafuta ndege kutoka nchi zingine ambapo ingeongeza gharama, kuchelewesha muda kusubiri ndege ifike na usumbufu wa vibali vya hiyo ndege ya nje”, amesema Magoti.

Amefafanua kuwa mzigo uliopakiwa na Air Tanzania utapelekwa hadi Dubai na kutoka hapo utasafirishwa kwenda Marekani kwa urahisi na uharaka kuliko wangetumia usafiri mwingine.

Mpango wa ununuzi wa ndege ya mizigo umelenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka na kuingia Tanzania na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post