Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewamasisha Maspika, Wabunge na Viongozi Wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za SADC kutembelea vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana nchini.
Mhe. Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 03, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za SADC jijini Arusha utakaomalizika Julai 08, 2023 uliojumuisha zaidi ya wajumbe 200 kutoka nchi mbalimbali wanachama wa SADC.
Amewahakikishia wajumbe hao kuwa Arusha ni eneo la kitovu cha utalii wa kimataifa ambapo wanaweza kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika hifadhi na kufurahia vivutio hivyo ambavyo vingine havipatikani katika maeneo mengi duniani.
“Naomba niwahakikishie kwa wageni ambao ni mara ya kwanza kuja nchini, Arusha ni sehemu nzuri ya kitalii kwa ajili ya kujionea vivutio vya utalii vya kimataifa.” Amesisitiza Mhe. Rais
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe hao kutembelea maeneo mengine ya Tanzania pindi wakimaliza mkutano huo kuwa ni pamoja na Zanzibar na maeneo ya kusini mwa Tanzania.
Akimkaribisha kufungua mkutano huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema jiji la kimataifa la Arusha limechaguliwa kufanyia mkutano huo kutokana na umuhimu wake katika masuala mengi ikiwa ni pamoja na kuwa kitovu kikuu cha kufikia maeneo yenye vivutio vya kipekee vya utalii kwa muda mfupi.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Arusha na Tarangile ambapo amesema kutokana na umuhimu huo ndiyo maana waziri mwenye dhamana ya utalii nchini, Mhe. Mohamed Mchengerwa pia ameshiriki katika mkutano huu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kuboresha utalii wa mikutano ili kuwavutia wageni kutoka maeneo mbalimbali duniani kuja nchini hivyo kuongeza pato na uchumi wa taifa kwea ujumla.
Aidha amefafanua kuwa kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la utalii kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mhe. Rais Samia katika Filamu ya The Royal Tour ambapo amemshukuru na kumpongeza kwa kazi hiyo ambayo amesema imezaa matunda makubwa kwenye sekta.
Amefafanua kuwa tayari Serikali inakwenda kujenga kumbi kubwa za kisasa kwa ajili ya utalii na ametoa wito kwa watanzania pia kuhamasika na kutembelea maeneo ya utalii ili pia kukuza utalii wa ndani.
Mada kuu ya mkutano ni kuboresha kilimo ili kutatua changamoto ya ukosefu wa chakula na ajira kwa vijana
Social Plugin