Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SENYAMULE KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI DODOMA

 

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule.


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

 

BAADA ya jiji la Dodoma kutajwa kuwa kinara wa migogoro ya ardhi nchini mkoa umezindua mkakati maalum wa kushughulikia tatizo hilo utakao tekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ukihusisha wataalam wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, amebainisha hayo jijini hapa wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kushughulikia tatizo la migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma.

 

Amesema tangu kutangazwa rasmi kwa mpango wa serikali kuhamishia shughuli zake makao makuu ya nchi Julai 25, 2016, jiji la Dodoma limeendelea kukua kwa kasi kubwa na kuvutia fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta zote muhimu.

Amesema sekta hizo ni pamoja na huduma za kijamii, kiuchumi, biashara, ujenzi na uwekezaji wa miundombinu msingi.

“Kwa mujibu wa makisio ya mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Jiji la Dodoma linakadiriwa kuwa na wakazi takribani 765,179 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 16.2 la idadi ya wakazi wote waliokuwepo mwaka 2016”amesema

Aidha, Senyamule amesema ongezeko hilo limesababisha uwepo wa mahitaji makubwa ya ardhi hususan la viwanja kwa ajili ya kukidhi matumizi ya shughuli za ofisi mbalimbali za umma na binafsi sambamba na biashara mpya zinazofunguliwa. 

“Kimsingi halmashauri ya jiji la Dodoma kama ilivyo kwa halmashauri nyingine hapa nchini kwa sasa ni moja ya halmashauri zinazokabiliwa na kero za migogoro mingi ya ardhi,”amesisitiza

Amesema kwa kuzingatia hilo kumekuwa na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichuliwa na halmashauri ofisi ya mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, kamishna wa ardhi mkoa pamoja na wizara ya ardhi na vyombo vingine vya utatuzi wa migogoro katika kuipatia ufumbuzi.

Kadhalika amesema kwa muda mrefu mamlaka mbalimbali za serikali zimekuwa zikijitahidi kutatua migogoro hiyo lakini imekuwa na kwamba uchunguzi uliofanywa na mkoa walibaini malalamiko mengi ni ya fidia na watu walioahidiwa kupewa viwanja mbadala.

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com