Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Josephy Charos akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni tarehe 19 Julai, 2023 kulia kwake ni Mwenyekiti wa AMCOSS hiyo Mohamed Nditi
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Lilian Gabriel akizungumza jambo na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni (hawapo pichani) wakati wa kikao baina ya bodi, menejimenti ya TFRA na wakulima hao tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Shimo Peter Shimo akizungumza na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni Mkoani Kilimanjaro walipotembelea ili kujua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo hususani katika tasnia ya mbolea tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa , Thobias Mwesigwa akizungumza na wakulima wa Amcoss ya Kaloleli ya mkoani Kilimanjaro walipowatembelea kusikia changamoto zao pamoja na kuwashauri namna bora ya kuendeleza kilimo ili kupata tija zaidi
Na Mwandishi wetu -Kilimanjaro
Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema haitavumilia udanganyifu wa aina yeyote kwenye tasnia hiyo iwe unafanywa na watumishi, wafanyabiashara au wakulima.
"Hatutakubali kuvumilia udanganyifu wa aina yeyote iwe ni kwenye vipimo, bei ya mbolea au viwango vya ubora".
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Bodi ya TFRA, Thobias Mwesigwa wakati wa kikao baina ya wajumbe, menejimenti na wanachama wa AMCOSS ya Kaloleni iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Mwesigwa ameeleza hayo baada ya mkulima Ramadhani Abdalla Mariki kuwasilisha ombi la kuwaagiza mawakala wa pembejeo za mbolea kuwa na mizani kwa ajili ya kupima mbolea ili kujiridhisha na uzito kama ulivyoandikwa kwenye vifungashio.
Aidha, mkulima Reward Shelukindo ameeleza uwepo wa baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu wanaouza mbolea kinyume na bei elekezi iliyotolewa na serikali ikiuzwa kwa kiasi cha shilingi 75,000 hadi 100,000 jambo ambalo bodi hiyo imeeleza kutokuvumilia jambo hilo na kueleza hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu hao wenye nia ovu.
"Wale waliobainika wamefanya udanganyifu msimu uliopita tunawafuta kwenye biashara ya mbolea lakini pia hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na wale waliosafi tutaendelea nao.
Mwesigwa amewataka wakulima na watanzania kwa ujumla kutoa taarifa pindi wanapobaini uwepo wa udanganyifu kwenye kilimo hususan kucheza na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na serikali kwa lengo la kuwakwamua wakulima na kuongeza uzalishaji.
"Mzee ukipata taarifa yoyote tupe tutaifanyia kazi. Naomba niwahakikishie wananchi kuwa changamoto hizo zitatatuliwa ili muweze kupata mbolea yenye viwango na kwa bei iliyotolewa na serikali", Mwesigwa alikazia.
Amewaomba wakulima kutoe ushirikiano kwa serikali, na kueleza kuwa, Bodi kwa kushirikiana na TFRA watajitahidi kutatua changamoto za wakulima hususan za kufikisha mbolea kwa wakulima kwa wakati.
Akieleza lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Josephy Charos amesema imelenga kuwatembelea wazalishaji, wanufaika ambao ni wakulima pamoja na wafanyabiashara ya mbolea ili kusikia changamoto wanazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, ameeleza kuwa, kufuatia Bodi kuwa na muda mfupi tangu iteuliwe imeona vyema kujifunza kwa vitendo na kupata uelewa wa kile wanachokisimamia kutokea chini kabisa.
Kwa upande wake Hadija Jabir Mjumbe wa bodi aliwashauri wakulima kuhakikisha wanapima afya ya udongo katika mashamba yao ili kuweza kutumia virutubisho sahihi kutokana na uhitaji uliojidhihirisha baada ya kupima.
Pamoja na hayo alitoa ushauri ka wakulima kutumia visaidizi vya udongo kama vile chokaa ili kuimarisha afya ya udongo na kuongeza mazao na tija kwenye kilimo.
Social Plugin