SERIKALI YATENGA BILIONI 54 KWA AJILI YA UJENZI WA VYUO VYA UFUNDI STADI VETA 65 NCHINI.

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu, Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta Anthon Mzee Kasore



Na Mwandishi Wetu, Tanga

SERIKALI imesema inaendelea na ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi stadi Veta utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 54 katika Mikoa na Wilaya hapa nchini, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inatoa elimu ya Amali itakayokidhi matakwa ya mabadiliko ya sera ya elimu. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda alisema hayo  alipotembelea chuo cha ufundi stadi Veta Jijini Tanga ili kujionea namna kinavyotoa mafunzo ya Ufundi Stadi lakini pia kuhakikisha wanatoa huduma zinazostahiki kwa jamii. 

Waziri Mkenda amesema kuwa kati ya vyuo 65 vinavyojengwa Nchini, Vyuo 64 ni za Wilaya na Chuo Kimoja cha Mkoa ambapo hadi sasa tayari imetoa kiasi cha shilingi bilioni 37 huku matumaini yakiwa makubwa katika kila maeneo yanayojengwa vyuo hivyo ambavyo ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. 

"Tukiwa bungeni swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa mara nyingi kuliko maswali mengine yote katika wizara ya elimu sayansi na teknolojia ni kuhusu veta kila mmoja anauliza ni lini veta itajengwa kwake watu wanamatarajio makubwa sana kwenye veta kwa maana hiyo sisi tuna kazi ya kuhakikisha tunakidhi matarajio yao kwa kutoa elimu ya amali ambayo ni bora na ambayo itakidhi matakwa ya vijana, "alisema Waziri Mkenda. 

Prof Mkenda amesema zipo namna mbili za kuendelea kuwapima wahitimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta ambapo moja ya njia ni kuangalia wahitimu wanafanya wapi kazi mara baada ya kuhitimu mafunzo yao na kuwahoji waliowaajiri namna walivyoridhika na utendaji kazi wao. 

Pia Waziri Profesa Mkenda aliwaagiza viongozi wa Veta kuhakikisha wanaandaa bajeti na kuiwasilisha wizarani itakayoomba fedha kwa ajili ya kununulia zana bora zinazokidhi teklonojia ya sasa katika karakana za Ufundi wa magari ili vyuo hivyo vya Veta viweze kuingia sokoni kutengeneza magari ya serikali, mashirika na watu binafsi.

Mkurugenzi wa Veta kanda ya Kaskazini Monica Mbele, alisema wamepokea maagizo hayo ambayo pindi wakipata nyenzo na zana bora za kisasa wataweza kuwa na utayari wa kutengeneza magari lakini pia kuongeza walimu wenye ujuzi wa teklonojia ya kisasa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Antony Mzee Kasore alisema watahakikisha wanakwenda kutekeleza maagizo ya Waziri ya utoaji wa mafunzo bora na kuhakikisha wanatoa mafunzo yanayohitajika na yanayozingatia ubora unahitajika. 

"Kama tulivyosikia kuna vyuo vinavyojengwa 65 katika wilaya mbalimbali na Mkoa na chenyewe pia tunakwenda kusimamia kama maelekezo aliyotoa ya kuhakikisha tunasimamia ujenzi huo uweze kufanyika tukiamini tutakuwa tumekwenda kutekeleza yale yote yaliyoanishwa, "alisema 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post