SERIKALI YAVIKUMBUKA VYUO VYA UALIMU NCHINI


Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Vyuo vya Ualimu nchini kwa kujenga majengo mapya, kukarabati pamoja na kuweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Akikagua utekelezaji wa Miradi ya Elimu katika Chuo cha Ualimu Kasulu na Kabanga yote ikiwa wilayani Kasulu Mkoani Kigoma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Franklin Rwezimula amesema lengo ni kuhakikisha walimu tarajali wanapata mafunzo katika mazingira bora.

Amesema maboresho hayo yamekwenda sambamba na kuweka mifumo inayotumia nishati asilia kupikia akitolea mfano Chuo cha Ualimu Kabanga ambacho kimejengewa mifumo hiyo na kupunguza matumizi ya kuni.

“Chuo cha Ualimu Kabanga ni kielelezo cha utunzaji wa mazingira katika ujenzi wa miundombinu yake kwa kuwa imewekewa mifumo ya kuchakata maji taka na kupata mbolea huku maji yakitumika tena kumwagilia na hapo hapo kupata gesi inayotumika kupikia,” amesema Dkt. Rwezimula

Nae Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Cosmas Mahenge amesema Chuo cha Ualimu Kabanga na kile cha Kasulu ni moja ya Vyuo vilivyonufaika na Mradi huo kwa kujengewa miundombinu mipya na kuwekewa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Amesema katika Chuo cha Ualimu Kabanga majengo yake yamejengwa upya na kuwa Chuo cha mfano katika kutunza mazingira kwa kuwa kinatumia biogas huku kile cha Kasulu kikijengewa maabara ya Fizikia, Kemia, Bailojia pamoja na Maktaba.

“Kwa ujumla Mradi huu ni mkombozi wa elimu ya ualimu kwa kuwa pamoja na kujenga na kukarabati umetoa mafunzo kwa wakufunzi, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA, vifaa vya kufundishia na kujifunzia,”ameongeza Mratibu Mahenge.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kabanga Edward Wawa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha ujenzi wa majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga na kuahidi kuleta ufanisi zaidi katika utendaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post