ZAWADI MSALLA- ZANZIBAR
Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe. mhandisi Zena Ahmed Said amewataka Taasisi zinazosimamia ununuzi wa Umma nchini Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA) kuhakikisha wanatoa mafunzo ya Sheria ya Ununuzi ipasavyo kwa watendaji wakuu wa Serikali ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wakati wa utekelezaji wa michakato ya ununuzi.
Mhandisi Zena ameyasema hayo leo alipokutana na bodi za Wakurugezi na menejmenti za Taasisi hizo mbili ofisini kwake Ikulu Zanzibar. Ameeleza kuwa eneo la ununuzi Serikalini ni kati ya aeneo lenye changamoto na linalohitaji kutolewa mafunzo ili kuhakikisha thamani ya fedha katika ununuzi inapatikana.
Amesema kuwa watendaji wakuu wa taasisi wanatakiwa kuhakikisha taratibu za ununuzi zinafuatwa na kuufahamu vizuri mchakato mzima wa ununuzi. Hii itasaidia katika kuhakikisha ununuzi unafanyika kwa haki, uwazi na thamani ya fedha inaonekana kwani zaidi ya asilimia sabini ya bajeti ya Serikali zote mbili imeelekezwa katika ununuzi.
“Watendaji wakuu wengi wamekuwa wakishindwa kufuata taratibu za michakato ya ununuzi hii ni kazi yenu kuhakikisha mnawapatia mafunzo stahiki ili kusaidia matumizi mazuri ya fadha ya Setrikali” Alieleza.
Pia, Mhandisi Zena amesema mafunzo hayo yanatakiwa kutolewa kwa bodi za zabuni ili kuhakikisha bodi hizo zinapitisha manunuzi kwa kufuata sheria ya ununuzi wa Umma na kanuni zake na kuelewa kitu wanacho kipitisha. Ameongeza kuwa bodi hizo za zabuni ni muhimu kusisitiziwa umuhimu wa kusoma nyaraka zote za zabuni kabla ya kupitisha zabuni yoyote.
Aidha, Mhandisi Zena aliitaka PPRA kuhakikisha inasaidiana kwa ukaribu na ZPPDA katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha Taasisi hiyo inakuwa kati ya Taasisi bora kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Alisema anatambua PPRA ni Taasisi kongwe kidogo ukilinganisha na ZPPDA na tayari imeshaisaidia Serikali kwa kiwango kikubwa katika masuala ya ununuzi.
“Nina fahamu hapo zamani PPRA mlikuwa mkitoa mafunzo, nina amini mpaka sasa bado mnatoa mafunzo, wapeni mbinu hizo ZPPDA za utoaji wa mafunzo, mmenieleza mmejinge mfumo mpya wa ununuzi ni wakati muafaka kwa ZPPDA Kwenda kujifunza na kuona ubora wa mfumo huo, ili walinganishe na mfumo walio nao na wanaoutumia kwa sasa” Alisema
Kwa upande wa PPRA mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Leonada Mwagike alimueleza Mhandisi Zena kuwa PPRA imejipanga kushirikiana na ZPPDA na ndiyo lengo kuu lililowafanya waweze kufika Zanzibar. Dkt. Mwagike alieleza kuwa tayari Taasisi hizo mbili zimeweka maazimio ya kusaini mkataba wa mashirikiano ambapo unatarajiwa kusainiwa ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Dkt. Mwagike alieleza mkataba huo utaangalia vipengele vyote muhimu vya utendaji ikiwemo kubadilishana uzoefu kwa watumishi wa Taasisi hizo mbili na kubadilishana ujuzi wa kutoa mafunzo ya sheria ya ununuzi wa umma.
Naye Mwenyekiti wa ZPPDA Dkt Sharifa Omar Salim alisema ujio wa Taasisi mwenza umeleta hari kubwa kwa upande wao na kuongeza kuwa wanaanimi mkataba watakao enda kuingia kati ya Taasisi hizi mbili utazaa matunda.
“Licha ya kwamba tayari Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alizitaka Taasisi zinazofanana kwa pande zote mbili kushirikiana sisi ZPPDA tumeona upendo na shauku waliyo nayo PPRA kuhakikisha taasisi zetu zinasonga mbele” Alisema
Social Plugin