Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TCRA SASA KUTOA MASAFA BURE KUWEZESHA MAWASILIANO YA WAZI KWA UMMA


*************

Na Mwandishi Wetu.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa ipo katika hatua za awali za kufungua bendi za masafa ambazo zitatumiwa na watoa huduma bure bila kuhitaji kuwa na leseni ya rasilimali masafa (Unlicensed bands). “Hatua hii itaongeza matumizi ya Intaneti kwa kuwa na huduma za intaneti za wazi (WiFi -hotspots” alieleza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dodoma wiki iliyopita.

Alisema kuwa, upangaji na usimamizi mzuri wa rasilimali za mawasiliano (masafa na namba), ndio unaowezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano pamoja na huduma za pesa mtandao na kwamba TCRA imefanikiwa kugawa masafa yanayowezesha utoaji wa huduma ya intaneti ya kasi na sasa imeweka mkakati wa kutoa masafa hayo bure ili wananchi waweze kuongeza matumizi ya huduma za intaneti.

“Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya Wananchi wanapata huduma ya intaneti ya kasi. Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kufungua fursa za milango ya TEHAMA ili kufikia lengo hili” alisisitiza Dkt Jabiri.

Mamlaka hiyo ilieleza kuwa, Rasilimali za mawasiliano ambazo inawajibika kuzisimamia ni pamoja na masafa, namba, vikoa, postikodi na anwani za makazi.

“TCRA imeendelea kuhakikisha uwepo wa rasilimali zinazowezesha mawasiliano ya simu, Intaneti, redio na televisheni. Usimamizi wa rasilimali hizi umeweza kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa” alisema Jabiri.

Kuhusu mgawanyo wa masafa mbalimbali Mkurugenzi Mkuu huyo alibainisha kuwa, TCRA imefanikiwa kutoa rasilimali masafa katika bendi za 700MHz, 2300MHz, 2600MHz na 3500MHz yaliyowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizoanza kutumia intaneti ya kasi ya 5G.

“Kuwepo kwa Intaneti ya kasi kunawezesha uchumi wa kidijiti katika maeneo mbalimbali kama vile Huduma za kifedha, utalii, kilimo na huduma za afya,” alibainisha.

Kuhusu masafa ya Utangazaji Dkt Jabiri alisema TCRA ilitangaza masafa ya utangazaji wa redio katika mikoa 21 ya Tanzania bara ambapo jumla ya watoa huduma thelathini (30) walipata nafasi ya kuanzisha vituo vya utangazaji wa redio katika maeneo mbalimbali ambapo hadi sasa Tanzania ina jumla ya vituo…..vya Utangazaji wa redio, vituo…..vya Utangazaji wa Televisheni vinavyotumia rasilimali ya masafa.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzaniza (TCRA) ndiyo taasisi yenye wajibu wa usimamizi wa rasilimali za mawasiliano ambazo ni masafa, namba, vikoa, postikodi na anwani za makazi. Mamlaka hiyo ina wajibu kwa mujibu wa Sheria za TCRA na Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2003 na 2010 mtawalia kusimamia rasilimali za mawasiliano ikiwemo kutoa leseni na kusimamia Matumizi ya rasilimali za mawasiliano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com