Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUMIENI MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI – WAZIRI DKT MABULA


Waziri wa Ardhi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa mkutano wa Wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya wilaya ya Longido tarehe 8 Julai 2023.

****************

Na Munir Shemweta, WANMM LONGIDO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametaka wananchi wa wilaya ya Longido mkoani Arusha kutumia fursa ya Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini kutatua migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu katika halmashauri hiyo.

Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 8 Julai 2023 wilayani Longido mkoa wa Arusha wakati akifungua Mkutano wa wadau kujadili Mpango wa Matumzi ya Ardhi wilaya ya longido uliobeba kauli mbiu ya uboreshaji milki kwa maendeleo endelevu.

Amesema, halmashauri ya wilaya ya Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo muingiliano wa aina za ardhi. Kwa mujibu wa Dkt Mabula changamoto hizo zimesababishwa na taasisi mbalimbali kufanya kazi katika eneo moja kwa nyakati tofauti pasipo kushirikiana.

‘’Pamoja na changamoto hizi serikali imelazimika kuichagua halmashauri ya wilaya ya Longido kuwa miongoni mwa halmashauri saba zinazotekeleza shughuli za urasimishaji ardhi ya vijiji kupitia mradi wa kuboresha usalama wa milki.

Amewataka washiriki wa mkutano huo kutumia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kama fursa na kuwataka viongozi na wananchi wa wilaya ya Longido kutoa ushirikiano thabiti ili kufanikisha utekelezaji wake.

‘’Maeneo mengi yalitamani kupata fursa kama hii lakini kutokana na uchache wa rasilimali hawakufanikiwa kufikiwa na mradi, nashauri tumieni fursa hii kikamilifu kwa maendeleo ya wilaya na mkoa wa arusha kwa ujumla’’. Alisema Dkt Mabula

Aliongeza kuwa, katika kuongeza juhudi za serikali kutatua changamoto zinazoikabili halmashauri ya wilaya ya longido, Wizara ya Ardhi imewezesha halmashauri hiyo kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wenye mapendekezo ya maeneo yaliyopaswa kubaki kuwa ardhi ya vijiji ikiwa ni pamoja na ardhi kwa ajili malisho, ardhi ya hifadhi na maeneo ya ardhi ya jumla.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mapendekezo hayo yamewasilishwa katika mkutano huo kujadiliwa kwa pamoja na kufanya maboreshio stahili ili mpango huo uwe unatambulika na kukubalika na wadau wote.

Awali Mkuu wa wilaya ya Longido Marco Ngumbi amewaambia washiriki wa mkutano huo,, kuwa makini wakati wa utekelezaji Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika halmashauri ya Longido huku akitaka kuheshimiwa kwa wataalamu pale linapofanyika suala la kitaalam. Alitoa tahadhari kwa viongozi wa halmashauri hiyo na kauli wanazotoa wakati wa utekelezaji wa mradi.

‘’Ni muhimu kwa viongozi kuwa na tahadhari ya kauli, maneno na mienendo pale linapotokea suala la utalaamu na kinachofanyika sasa katika mradi siyo kipya kilifanyika katika serikali za awamu zote kuanzia ya kwanza hadi ya sasa’’ alisema Ngumbi .

Meneja Urasimishaji Ardhi ya Vijiji kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Joseph John Osena amesema, mkutano huo wa Wadau kujadili Mpango wa Matumizi ya Ardhi unatoa fursa kwa wadau kujadiliana kuhusu mpango sambamba na kuwa na usalama wa maeneo yao.

‘’Kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki hati zinaenda kutolewa katika vijiji na srerikali inataka kuona wananchi wake wako salama na Longido ni moja ya wilaya chache zinazofikiwa na mradi’’ alisema
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya wilaya ya Longido tarehe 8 Julai 2023.
Mkuu wa wilaya ya Longido mkoa wa Arusha Marco Ngumbi akizungumza katika mkutano wa Wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya wilaya ya Longido tarehe 8 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa mkutano wa Wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya wilaya ya Longido tarehe 8 Julai 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com