Na.Mwandishi Wetu_ARUSHA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka nchi za kiafrika kuongeza ushiriki wa wanawake katika majukwaa ya maamuzi ikiwa ni moja ya njia za kuelekea kwenye usawa wa kijinsia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa AWLO jijini Arusha Julai 06, 2023 Dkt. Gwajima amesema kuwa moja ya vikwazo vikuu kufikia usawa wa kijinsia ni sekta ya elimu kwani wanawake hawapati nafasi sawa ya kujiendelea kielimu.
Ameshauri kuongeza fursa sawa za kupata elimu kwa wanawake na wanaume ili kufikia malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia katika nchi za Afrika.
Dkt. Gwajima amezungumzia fursa za kiuchumi kuwa na nafasi kubwa katika kufikia malengo ya usawa wa kijinsia kwani jamii yenye uchumi imara inaweza kutoa fursa sawa kwa jinsia zote katika elimu, biashara na fursa nyingine zinazopatikana kwenye jamii husika.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Gwajima amebainisha kuwa kufikia usawa wa kijinsia siyo suala la kuchagua bali ni swala la lazima na kwamba kila nchi iangalie namna ya kuondoa vikwazo vyote vinavyosababisha kuchelewesha kufikia usawa wa kijinsia na kuviondoa.
Awali akiwakaribisha washiriki wa mkutano huo, mwanzilishi na rais wa AWLO (African Women in Leadership Organization) Dkt. Elisha Attai amesema kuwa kwa sasa bado wanawake wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazosababisha washindwe kufikia mafanikio katika majukumu wanayotekeleza kila siku kwenye kazi zao kwa sababu tu ni wanawake.
Social Plugin