Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WAFURAHIA PROGRAMU YA JENGA KESHO ILIYO BORA ‘BBT’ INAVYOLETA MAPINDUZI KATIKA KILIMO

Na Nyabaganga Daudi Taraba

Vijana 820 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, ambao wamehitimu mafunzo yao katika vituo atamizi mbalimbali hapa nchini (Vyuo vya Kilimo), wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tamzania kwa mpango huo mzuri wa kuwapa vijana ajira kupitia kilimo.


Wakizungumza na mwandishi wetu baada ya kuhitimu mafunzo ya kilimo kwenye vituo atamizi vijana hao wameeleza kufurahishwa na kile ambacho Programu ya BBT imelenga.

Janeth Fredrick Moshi kutoka Mkoa wa Manyara aliyekuwa kituo cha KATC Moshi anasema “Kwa kweli nimejifunza mengi, ila hili la kuanzia sokoni kisha nirudi shambani kuzalisha, nimetoka nalo, kwani hapo awali nilikuwa nazalisha chochote na mwisho wa siku sipati soko. Lakini kwa sasa lazima nifanye utafiti kwanza wa hali ya soko ndipo nizalishe, na hicho ndicho Kilimo Biashara”.


Aidha, ameiomba serikali iendelee kutoa mafunzo kwa vijana wengine, maana huo ni ukombozi wao.

Ameshukuru kwani amefundishwa kilimo bora kwa sababu alizoea kilimo cha mazoea hivyo ameahidi kuwafundisha vijana wenzake.

Revina Dastan kutoka Mkoa wa Mwanza anasema “Nimejifunza mazuri maana nimelima mwenyewe na nimekabiliana na changamoto za shambani, hivyo kuna kitu nimejifunza sana. Namshukuru Rais wetu na namshukuru sana Waziri wetu wa Kilimo kwa fursa hii. Vijana twende kulima, tutumie mitandao kwa faida. Tusipoteze muda, tuache kukaa vijiweni, Kilimo kina pesa”.

Naye Papaye Njiday kutoka Mkoa wa Manyara aliyekuwa kituo atamizi cha Horti Tengeru ameomba programu iwe endelevu, iwaguse vijana wengi. Hili likifanikiwa kufikia wengi kutakuwa na mapinduzi ya kilimo hapa nchini na nchi zingine zitalishwa chakula kutoka Tanzania.

“Hii ni fursa ya pekee, yaani kama ningekuwa na elimu hii tangu awali ningekuwa mbali. Elimu hii ya kilimo ipelekwe shuleni na vyuoni pia”,amesema.

Amewataka vijana wachangamkie kilimo na kwamba ataajiri vijana na kutoa elimu kwa wale ambao hawakupata nafasi hiyo.

Aidha, ameishukuru serikali kwa mpango huo.

Daud S. Laizer kutoka Arusha, Sada Omary toka Dodoma, Rabia Mtega Alkariti na Naomi Lau toka Dar es Salaam, Bishwa Ngonga Alphonce toka Mkoa wa Kigoma, Neema Samsoni Katumba kutoka Mkoa wa Geita na Phares Chacha kutoka Mkoa wa Katavi, kwa niaba ya wenzao ambao hawakupata nafasi katika mahojiano hayo, Kwa nyakati tofauti walipohojiwa, wameonesha kufurahishwa na program hii ya BBT.
Wamempongeza Mbeba Maono hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mtekeleza Maono ya BBT, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, na wote wanaohusika katika programu hiyo.

Wanashauri vijana kuangalia fursa iliyoko katika kilimo kwani kinalipa, waache mazoea ya kukipa kilimo nafasi ya mwisho, wakipe nafasi ya kwanza, maana ni uti wa mgongo kuna chakula, malighafi na ajira katika kilimo.

Wamesema Kilimo ni fursa, kinalimwa shambani, siyo kwenye mitandao, watoke ardhi ipo, watoke wakalime kwani wasipotoka hawataona mashamba na kwamba kuna maeneo yana ardhi ya kutosha, lakini vijana bado wanalalamikia ajira.

“Tutoke vijana, fedha ziko kwenye kilimo”,wamesema.

Vijana wa kike wao pia wameshukuru kukumbukwa katika programu. hiyo.

“Mafunzo tuliyopata ya kilimo yapelekwe shuleni na vyuo vyote. Vijana wenye elimu ya darasa la saba na wasio na elimu nao pia wakumbukwe, hususan wale ambao tayari wamejikita kwenye kilimo. Watapata kitu kama sisi tulivyopata. Kule vituoni, mafunzo yaliyotolewa asilimia 80 ni vitendo na asilimia 20 ndiyo nadharia, hivyo wataweza”,wameeleza.

Wamesema watakuwa mabalozi kupeleka kile walichopata kwa wakulima wengine.

Aidha wameshukuru kwa mpango huo uliokumbuka makundi haya ya vijana, wanawake na walemavu huku wakisema kazi iendelee kwa kufikia lengo la AGENDA 10/30.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com