HEROIN NA BANGI ZANASWA KATIKA OPERESHENI MAALUM MKOANI IRINGA

 

Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imefanya  operesheni maalum katika mkoa wa Iringa na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 276 za dawa za kulevya aina  heroin  na bangi na kuwakamata jumla ya watu 12 wakihusishwa na dawa hizo.


Akitoa taarifa  kwa niaba ya Kamishna Jenerali  leo tarehe 27 Agosti 2023 Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka  hiyo   Daniel Kasokola  , ameeleza kuwa lengo la operesheni hizi ni kuvunja na kusambaratisha mitandao yote ya  wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuwakamata  wote wanaojihusisha kwa namna yoyote na dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.


“Operesheni hizi ni moja ya utekelezaji wa mkakati  wa kudhibiti upatikanaji wa dawa za kulevya (Supply Reduction), hivyo kama Kamishna Jenerali   anavyoeleza operesheni hizi zitafanyika nchi zima,   tuwahakikishie tutawakamata vinara wote  wanaojihusisha kwa namna  moja au nyingine na kilimo au biashara ya dawa za kulevya kwani mitandao yao na mbinu zao tunazijua hivyo hakuna mhalifu wa dawa za kulevya ambaye ataukwepa mkono wa sheria”


Aidha, ameeleza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na dawa za kulevya nchini, hivyo,  kwa sasa Tanzania siyo sehemu salama kwa wote wanaojihusisha na biashara au kilimo cha dawa za kulevya. Hivyo watanzania waungane na serikali katika mapambano  haya kama walifanya  wananchi wa Kisimiri juu, Lesinoni na Lenglong  mkoani Arusha na wananchi wa walaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuamua  kwa hiari yao kuondoa mimea ya bangi na mirungi katika maeneo yao.


Pia, amesema kuwa, Dawa dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa Taifa letu zikiwemo  za kiafya, kijamii, kiuchumi, kiusalama na kidiplomasia. Hivyo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  juu ya watu wanaojihusisha na kilimo na biashara ya dawa hizi za kulevya kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupiga simu ya bure namba 119.

Ameendelea  kufafanua kuwa, katika kukahakikisha  dawa za   dawa za kulevya zinazibitiwa, Sheria ya Kudhibiri  na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015  inatoa adhabu kubwa kwa wale watakaotiwa hatiani kwa  makosa hayo, adhabu yake inaweza  kufikia   kifungo cha maisha cha miaka 30 jela hadi  kifungo cha maisha pamoja  kutaifishwa kwa mali zote za mshtakiwa ambazo zitathibitika alizipata katika kipindi cha miaka 10 tangu akamatwe.

Akizungumzia operesheni hiyo Mtendaji wa kata ya Malolo wilaya ya Kilosa Fredinand Litweka  ameshukuru  kufanyika kwa operesheni hiyo  katika  maeneo hayo kwani yameshamiri kwa kilimo cha bangi na kuongeza kwamba, uongozi wa wilaya umekuwa wakifanya jitihada kadhaa bila mafanikio hivyo, kufika kwa mamlaka katika maeneo yao kumeongeza chachu ya mapambano dhidi ya kilimo na biashara ya dawa za kulevya.


Nao  wakazi wa Ruhaa Mbuyuni, akiwemo  Jefari Jeda wameeleza kuwa, wanaunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa jitihada zaidi zifanyike kuhakikisha wanawakamata wote wanaojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya kwani madawa haya yana madhara makubwa. Wameeleza kuwa,  wako tayari kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuonesha mashamba yaliyolimwa bangi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post