Naibu Waziri wa Madini Dkt. Stephen Kiruswa amesema kutokana na kuwapo kwa changamoto za wawekezaji katika zao la chumvi nchini, Serikali imeagiza Shirika la Madini STAMICO kujenga kiwanda wilayani kilwa mkoani Lindi, ili kutatua changamoto za wazalishaji wadogo wanaolima chumvi katika mikoa ya kusini.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Agost 21,2023 katika kongamano la wadau wa Sekta ya Chumvi lenye lengo la kujadili kwa pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
Ameeleza kuwa Viwanda vya Chumvi vitkijengwa kutaondoa kwa kiasi kikubwa changamoto zilizopo za wazalishaji wadogo wa sekta hiyo, na kuweza kufikia malengo yao ya kibiashara na kuchangia katika pato la Taifa,
Kwa uapnde wake Meneja uwezeshaji wachimbaji Madini Taifa, Tuna Bandoma, amesema kuwa Kongamano hilo limelenga kutatua changamoto za Wadau wa Chumvi na kwamba, serikali imekuwa na mikakati mbalimbali kuhakikisha soko la chumvi linapatikana.
“Chumvi imekua ni kilio kikubwa na changamoto kubwa, lakini serikali ina mkakati mkubwa kuhusu soko la chumvi, na kongamano hili limekuja kuwajengea uwezo wadau ili tujadili tunajikwamua Vipi katika sekta ya chumvi” amesema.
Aidha ameongeza kuwa, katika maonesho hayo wamealika viwanda vinavyozalisha chumvi, ili kuwapa elimu wazalishaji wadogo wazingatie ubora utakaokuza soko, huku mkuu wa mkoa huo Zainab Telack akieleza kuwa mkoa huo una fursa za madini ya aina zote.
Mwenyekiti wa kamati ya madini ya chumvi Abdalah Ismaila, ameiomba serikali kuharakisha inatekeleza ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani chumvi ukanda wa kusini, ambapo bidhaa hiyo imekua ikitumika ikiwa ghafi.
Naye, katibu wa chama cha uzalishaji chumvi Tanzania Julis Mosha, amesema wazalishaji wameathirika Kwa kiasi kikubwa Kwani wamekua wakizalisha kwa hasara kutokana na kukosa soko la uhakika la kuuza chumvi.
Kongamano hilo la siku moja lilikuwa na watoa mada mbalimbali kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, Nilkant, Sealsalt , Benki ya NMB , CRDB na NBC, ambapo kwa pamoja wamewezesha kufanikisha Kongamano hilo, ikiwa ni sehemu ya matukio yanayofanyika katika Maonesho ya Madini na Uwekeaji yaliyofunguliwa leo na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Stephen Kiruswa kwenye viwanja vya kilimahewa wilayani Ruangwa mkoani lindi.