Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda (kushoto)akikabidhi Kompyuta kwa wanafunzi ambazo zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi (kulia).
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi, ametoa Kompyuta 10 kwa shule tatu za Sekondari Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya Masomo ya TEHAMA.
Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu amekabidhi Kompyuta hizo leo Agosti 26, 2023 kwenye Mkutano wa hadhara Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT) uliofanyika katika Viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga.
Amesema ametoa Kompyuta hizo ikiwa ni mwendelezo wa zoezi lake la kutoa Kompyuta katika Shule za Sekondari Manispaa ya Shinyanga ili kusaidia katika masomo ya TEHAMA.
“Nimetoa Kompyuta 10, Projector 10, Printer 10,Monitor 10, Ups 10 kwa shule za Sekondari tatu ambazo ni Ndala, Chamaguha, na Shule mpya ya Wasichana Butengwa, vifaa hivi thamani yake ni milioni 30,”amesema Katambi.
Aidha, Katambi ametoa Mipira 20 yenye thamani ya Sh.milioni 1.6 kwa ajili ya kuunga mkono Mashindano ya UVCCM Shinyanga Mjini ya Dr. Samia Cup' maarufu Samia Viwanjani ambayo yatashirikisha timu 32 ambapo pia ametoa Sh. milioni 5 ikiwa ni zawadi kwa washindi watakaopatikana katika mashindano hayo.
Katika hatua nyingine amewaomba wananchi wa Shinyanga waachane na wanasiasa wababaishaji, wapiga porojo na wenye kujali maslahi yao binafsi, bali wamuunge mkono ili aendelee kuwaletea maendeleo.
Aidha, amewataka pia wananchi wa Shinyanga waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba kupitia Rais pamoja na viongozi wa Chama, atazidi kuipaisha Shinyanga na kufikia lengo lake la kuiletea maendeleo, kwa kuongeza miundombinu itakayochochea mzunguko wa fedha, fursa za ajira, mitaji, biashara na uwekezaji.
Naye Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda, ambaye akikabidhi Kompyuta hizo kwa Walimu na Wanafunzi, amempongeza Mbunge Katambi kwa kujali elimu na hata kutoa vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia wanafunzi katika masomo yao na kufanya vizuri kitaaluma.
Nao baadhi ya Walimu ambao wamepokea vifaa hivyo wameshukuru ambavyo vitakuwa msaada mkubwa kwao katika kuongeza ufanisi wa ufundishaji.
Social Plugin