SENDEU AKABIDHI ZAWADI YA GARI, NYUMBA MWENYEKITI MSTAAFU WA KIJIJI....ATAKA JAMII KULINDA NA KUHIFADHI ARDHI


Mkurugenzi wa Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Rubby ijulikanayo kwa jina la Sendeu Agrovet Investment Limited,Gabriel Sendeu Laizer (wa kwanza kushoto) iliyopo katika kijiji cha Elesin'geta , kata ya Mundarara wilayani Longido mkoani Arusha akimkabidhi mwenyekiti mstaafu wa Kijiji hicho Akwelino Nikeni kadi ya gari aina ya Noah kama zawadi ya kurudisha fadhila kwa ajili ya utendaji kazi wake mzuri wakati wa uongozi wake tukio hilo lilifanyika kijijini hapo
Wananchi wa Kijiji cha Elesin'geta kilichopo katika kata ya Mundarara wilayani Longido mkoani Arusha wametakiwa kuhakikisha wanatetea ,kuhifadhi na kutunza ardhi yao kwa manufaa ya vizazi vijavyo kwani binadamu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki.


Hayo yamebainishwa na mkurugenzi wa kampuni ya uchimbaji wa mdini ya rubby ijulikanayo kwa jina la Sendeu Agrovet Investment Limited,Gabriel Sendeu Laizer
wakati akiongea katika sherehe za kumsimika mwenyekiti wa kijiji hicho mstaafu kuwa chifu wa Ukoo wa Kipuyo (Legwanani) pamoja na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uongozi wake ikiwemo ya kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho kupata maeneo ya kuchimba madini hayo ya rubby.


Alisema kuwa ni vyema wananchi wa Longido wakaendelea kulinda na kuhifadhi vyema ardhi yao kwa ajili ya kuvihifadhia vizazi vijavyo kwani iwapo wataitumia vibaya watasababisha watoto watakaozaliwa halo baadaye kukosa ardhi ya kutumia.


Aidha aliwataka vijana kufanya kazi kwa bidii , kuhifadhi na kutumia fedha ambazo wanazipata katika kazi zao vizuri katika kufanya shughuli za maendeleo na sio kufanya anasa ili kuweza kujikwamua katika wimbi la umaskini na kuliongezea pato taifa.

"Niwasihi pia vijana ambao mpo hapa mnaofanya shughuli zenu ikiwemo za uchimbaji madini mtumie fedha hizo vyema Kwa ajili ya maendeleo na sio mmalizie kwa wanawake pamoja na kunywa pombe ,mkitumia vyema itawasaidia nyie wenyewe pamoja na vizazi vyenu pia itamsaidia kuongeza pato la taifa", alisema Sendeu.


Aidha pia Seneu alimshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuwapatia wananchi wa wilaya hiyo maeneo kwa ajili ya kuchimba madini hayo ambapo alisema kuwa maeneo hayo yameweza kuwapatia vijana wengi ajira na kuwaondoa kabisa katika umaskini


"Nimshukuru pia katibu Mkuu wa taifa wa CCM  Daniel Chongolo pamoja na Waziri wa madini Dkt. Doto Biteko kwakuwa wao wamesaidia sana sisi wananchi wa Longido kupewa maeneo haya kwa ajili ya kufanya kazi hii ya uchimbaji ambayo kwakweli imesaidia sana vijana wengi kupata ajira",alisema Sendeu.


Katika  kutambua mchango wa Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji hicho wa kufanya kazi nzuri katika kipindi cha uongozi wake, Sendeu alimkabidhi nyumba aliyomjengea pamoja na gari aina ya Noah aliyomnunulia kwa ajili ya shukrani.


Akitoa shukrani zake mwenyekiti hiyo mstaafu wa Kijiji hicho Akwelino Nikeni aliwashukuru sana wananchi kwa namna walivyotambua mchango wake alioutoa wa kusaidia jamii katika kipindi cha uongozi wake ambapo aliwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano hata katika kipindi ambacho hayupo katika uongozi.


"Nimshukuru sana Sendeu kwa kunipa gari hii niahidi tu gari hii mbali na matumizi yangu binafsi pia litatumika kuwasaidia wananchi wa kijiji hiki na kata hii pindi watakapokuwa na uhitaji wowote pia nyumba hii itanisaidia kuishi mimi na familia yangu", alisema Nikeni.


Naye mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli Isack Copriano aliwataka wananchi wa wilaya ya Longido kushirikiana kutunza udongo wa Tanzania maana hakuna hazina nyingine yoyote iliyopo au watakayoweza kupata zaidi ya ardhi.


Alimpongeza Sendeu kwa kazi nzuri anayoifanya na kusema kuwa kazi kubwa ya mzalendo ni kuajiri vijana bila kuangalia mradi awe ni kijana wa kitanzania huku akimtaka kuendelea kuonyesha watanzania upendo na aendelee kusaidia serikali kuwapatia vijana ajira kwa ajili ya maendeleo pamoja na taifa kwa ujumla .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post