WATOTO WAWILI WAUAWA KWA KUNYONGWA, BABA YAO AKUTWA AMEJIUA JUU YA MTI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu ACP Edith Swebe

Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog Simiyu

Watoto wawili wa familia moja wameuawa kwa kunyongwa na kisha kuning'inizwa chumbani walimokuwa wakilala na wazazi wao katika kijiji cha Mwantemi kata ya Kinamweli wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu ACP Edith Swebe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa limetokea leo Ijumaa Agosti 11,2023 majira ya saa moja asubuhi ambapo mwili wa baba wa watoto hao pia aitwaye Bundu Ng'habi (32) umekutwa ukiwa unaning'inia juu ya mti.

"Katika tukio hili watoto wawili wamekutwa wamening'inizwa kwenye chumba wanacholala na wazazi wao na dalili zinaonesha kabisa kwamba watoto hawa wamenyongwa, lakini pia baada ya uchunguzi tumegundua baba mzazi wa aitwaye Bundu Ng'habi mwenye umri wa miaka 32 , mkulima mkazi wa Kinamweli naye alikutwa mwili wake ukiwa umening'inia juu ya mti mrefu  jirani na uzio wa nyumbani kwao, kwa tukio la huyu baba mzazi baada ya uchunguzi wa daktari tulibaini kuwa yeye amejinyonga" ,amesema kamanda Swebe.

Aidha kamanda Swebe amesema kuwa jeshi la polisi mkoani humo linaendelea kumtafuta mke wa marehemu ambaye mpaka sasa hajulikani alipo.

"Jeshi la polisi linaendelea kuchunguza na kumtafuta mke wa marehemu ambaye wakati wote wa tukio hakuwepo na hakuweza kupatikana na tunatoa wito kuendelea kumtafuta lakini pia kuendelea kuchunguza ili kubaini chanzo cha tukio hilo la kusikitisha." amesema kamanda Swebe.

Katika hatua nyingine kamanda Swebe ametoa wito kwa wananchi mkoani Simiyu  kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi mkoani humo kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubaini chanzo cha tukio hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post