Mwenge wa Uhuru 2023 umekagua , kutembelea na kuzindua jumla ya miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 10 wilayani Karagwe Mkoani Kagera.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na mbio za Mwenge katika wilaya hiyo ni pamoja na mradi wa shamba la miti Kigarama,mradi wa vijana wa bodaboda, vyumba vya madarasa Katembe, kuzindua jengo la huduma za upimaji na utengamano zahanati ya Kishoju, kiwanda cha kuchakata Maziwa cha Kahama Fresh na mradi wa maji Bisheshe .
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa 2023 Abdallah Shaib Kaim baada ya kukagua na kutembelea kiwanda cha Kahama Fresh amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili waweze kufanya uwekezaji wenye tija.
Amempongeza mwekezaji wa kiwanda cha Kahama Fresh kwa kutengeneza ajira zisizopungua 300 kwa vijana wa kitanzania kupitia kiwanda hicho.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda cha Kahama Fresh Josam Ntangeki amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata maziwa lita elfu 10 kwa siku na maziwa hayo yatakusanywa kwa wafugaji wanaozunguka mkoa wa Kagera na wataanza hivi karibuni.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho ni mkombozi kwa wafugaji kwani wataweza kuwa na soko la uhakika la maziwa kwa wafugaji wa ndani na nje na wanategemea kutoa ajira zisizopungua mia tatu kwa vijana wa Kitanzania.
Aidha amesema kuwa kiwanda hicho kimeshaanza program maalum ya kopa Ng'ombe lipa Maziwa na tayari wameanza zoezi hilo kwa kukopesha ngombe mia tatu tangu mwaka jana na baada ya mwaka mmoja mfugaji anakuwa ameshamaliza deni lake na kubaki na n'gombe.
Social Plugin