Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSEVENI ATUPWA JELA MIAKA 30 , KUCHAPWA VIBOKO 10 KWA KUMBAKA MTOTO WAKE "ALIMLEWESHA"


Na MWANDISHI WETU MALUNDE 1 BLOG

Mkazi wa Mtaa wa Nyasubi katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Mseveni Mchele Derefa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, viboko 10 na faini ya Shilingi milioni 1 na Mahakama ya Wilaya ya Kahama baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka 12.


Hukumu hiyo imetolewa juzi na Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Edmund Kente baada ya kuridhika na Ushahidi uliotolewa na Jamhuri ambao umethibitisha kosa hilo, pasipo kuacha shaka kuwa Mseven alitenda kosa hilo.


Amesema Mahakama imemtia hatiani kwa mujibu wa kifungu namba 130 kifungu cha 1, 2 (e) na 130 (1) vya Kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marejeo ya Mwaka 2022 ambapo Mseveni atatumikia kifungo cha Miaka 30 jela viboko 10 na faini ya Shilingi milioni moja.

Alifafanua kuwa Mahakama imetoa adhabu hiyo kwa Mseven ili iwefundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kwenye jamii ambao wanatekeleza matukio ya ukatili kwa watoto huku wakijua vitendo hivyo vipo kinyume cha Sheria.

Awali akisoma Shauri hilo la jinai namba 135 la Mwaka 2023 Wakili wa Serikali aliyekuwa anasimamia shauri hilo, Jukael Jairo aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa Mseveni ili iwe fundisho kwake na kwa wazazi wengine wanaotekeleza matukio ya ukatili kwa watoto wao.

Naye Mseven katika utetezi wake aliiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa madai kuwa anafamilia ya watoto watano wanaomtegemea, hoja ambayo ilitupiliwa mbali na Mahakama na kupatia adhabu hiyo.

Ikumbukwe kuwa Mseveni alituhumiwa kutenda kosa hilo Aprili 15 Mwaka huu kwa kumbaka mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka 12 Mwanafunzi darasa la saba shule ya Msingi Nyasubi kwa kumlaghai kwa kumpatia Chipsi na Kinywaji kilichochanganywa na Kilevi akimwambia ni dawa ya kutibu tatizo la UTI.

Kitendo hicho alikuwa akikifanya baada ya mke wake kusafiri kwenda mkoani Morogoro kumpeleka mtoto wake kwenye Matibabu na kumwachia binti huyo nyumbani huku taarifa za kufanyiwa ukatili huo zilitolewa na Majirani waliokuwa wakisikia kelele za binti kuingiliwa na Baba yake nyakati za usiku.

soma pia:

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com