Na Mariam Kagenda - Kagera
Mkoa wa Kagera tayari umepokea Mwenge wa uhuru leo Agosti 8,2023 kutoka mkoa wa Geita ambao wamehitimisha mbio za Mwenge na kuukabidhi mkoa wa Kagera.
Makabidhiano ya Mwenge wa uhuru kati ya mkoa wa Kagera na Geita yamefanyika katika kata ya Nyakabango wilayani Muleba mkoani Kagera ambapo mwenge huo utaanza kukimbizwa katika wilaya ya Muleba .
Wakati akipokea Mwenge huo mkuu wa mkoa wa Kagera Mh Fatma Mwassa amesema kuwa hali ya usalama katika mkoa huo ni salama na mwenge wa uhuru utakimbizwa katika halmashauri zote nane za mkoa huo kwa umbali wa Kilomita 1200.4.
Amesema kuwa mkoa wa Kagera utawapa ushirikiano wa kutosha wakimbiza mwenge kitaifa mpaka pale mkoa huo utakapohitimisha mbio za mwenge na kuukabidhi mwenge huo mkoa wa Geita Agosti 16 ,2023 ambapo ukiwa mkoani Kagera utazindua,kukagua,kutembelea jumla ya miradi 57 yenye thamani ya shilingi Bilioni 26.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigera wakati akikabidhi mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema kuwa mwenge wa uhuru ulipokuwa katika mkoa huo uliweka mawe ya msingi,kufungua,kuzindua na kukagua jumla ya miradi 59 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 29.