RC FATMA MWASSA ATEMBELEA NA KUKAGUA SHULE MPYA NYAKAHITA

Na Mariam Kagenda - Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amefanya ukaguzi ujenzi wa vyumba 16, jengo la utawala na matundu 18 ya vyoo shule mpya ya awali na Msingi Nyakahita iliyopo Kata ya Kanoni wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera.


Akiongea na wananchi wa kata hiyo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule amewataka wananchi waendelee kumtumia Mbunge ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa katika kuwaletea maendeleo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye dira yake ni kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu bure

Mhe. Mwassa amesema kuwa anaona leo wanaweza kuwa na madarasa mazuri mwanafunzi wa chekechea kutembea umbali wa kilometa 8 kwenda na kurudi sawa na kilometa 16 sio suala la kawaida kwa mtoto wanachoka sana , sasa Serikali imewasikia kinachobaki ni kuhakikisha watoto wote katika kijiji hicho wanapata haki yao ya kusoma na kuzifikia ndoto zao.


Mkuu wa wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer ameeleza kuwa kutokana na wananchi wa Kijiji hicho kuwa na uhitaji wa shule mara baada ya kupokea fedha kutoka Serikalini walijitoa kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo kwa kuchimba msingi, kusafisha eneo na kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.


Naye mmoja wa wananchi wa kijiji cha Nyakahita Novath Ndibalema amesema kuwa kabla ya ujenzi huo wananchi waliamua kujenga vyumba vya udongo ili kuwanusuru watoto wadogo ambao walitembea umbali mrefu kwenda shule kwani wanafunzi hao walilazimika kuamka saa 10:30 alfajiri ili kuwahi masomo hivyo ukamilishaji wa shule hiyo na usajili wa wanafunzi utarahisisha mwendo kwa watoto wao na kupunguza wasiwasi ambapo watakaosajiliwa katika shule hiyo wanaotoka mbali hawatazidi kilometa moja.


Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyakahita Mtungi Tirutangwa ameeleza kuwa shule mama ina wafunzi 1765 kuanzia darasa la nne hadi la saba na shule shikizi ina wanafunzi 218 kuanzia chekechea hadi darasa la tatu huku ufaulu wa shule hiyo ni asilimia 60, hivyo anaamini uwepo wa shule mpya utaongeza ufaulu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post