Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TGNP YAKUTANA NA ASASI ZA KIRAIA, VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA MAFUNZO YA UFUATILIAJI WA MZUNGUKO NA UCHAMBUZI WA BAJETI MRENGO WA KIJINSIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Lilian Liundi
                           ***

Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) umewaleta pamoja wawakilishi kutoka asasi za kiraia na vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini kwenye mafunzo ya ufuatiliaji wa mzunguko wa bajeti na uchambuzi wa bajeti ili kuhakikisha zinakuwa na mrengo wa jinsia na zinazingatia mahitaji ya makundi yote katika jamii.


Mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia leo tarehe 05 hadi 06 Agosti yanafanyika katika ofisi za TGNP zilizopo Mabibo jijini Dar es Salaam.


Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo leo Jumamosi Agosti 5,2023 ,Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Lilian Liundi amesema katika mafunzo haya ni muhimu katika ufuatiliaji wa mzunguko wa Bajeti pamoja na uchambuzi wa Bajeti katika mrengo wa kijinsia katika ngazi ya vijiji na kata kwa vituo vya taarifa na maarifa pamoja na baadhi ya asasi za kiraia.


Amesema warsha hiyo imejumuisha washiriki kutoka asasi za kiraia, vituo vya taarifa na maarifa kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Manyara, Mara, Kigoma, Morogoro, Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro, Mbeya na Shinyanga.


Amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa uchambuzi wa Bajeti pamoja na mzunguko wa Bajeti katika vijiji na kata wanapotoka ili kukuza uelewa wa dhana za jinsia na bajeti kwa mrengo wa kijinisa pamoja na kushirikishana mbinu za uchambuzi wa Bajeti yenye mrengo wa kijinsia.


“Mwaka wa fedha 2023/24 ni mwaka wa tatu wa utekelezaji Mpango waTatu wa maendeleo wa miaka mitanowa taifa 2021/22 hadi 2025/2026 wenye dhima ya Kujenga uchumi shindani na Viwanda kwa maendeleo ya Watu ambapo mpango huu una maeneo matano mkuu ambayo ni kuchochea uchumi shindani shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa viwanda na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara kuchochea maendeleo ya watu pamoja na kuendeleza rasilimali watu”, amesema Liundi.


"Mwaka uliopita 2022/23 kama taifa ulianza mchakato wa kutathmini dira yetu ya maendeleo ambayo inategemea kuweka kikomo ifikapo mwaka 2025 na mwaka huu umeanza mchakato mpya wa kutengeneza dira mpya ya taifa ya maendeleo yaani Dira ya Maendeleo Endelevu 2050 (Tanzania Development Vision 2050) uliozinduliwa Aprili 2023 ambapo dhima ya mjadala wa Bajeti ya Taifa unalenga kuchachua mjadla juu ya umuhimu wa Bajeti yenye mrengo wa Kijinsia katika kuchochea uchumi jumuishi",ameongeza.


Amesisitiza kuwa mwaka 2024 kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo kama wananchi wanatakiwa kujiandaa na kutengeneza vipaumbele vya kimaendeleo kwa hao watakaoweka nia ya kuwa viongozi wetu katika ngazi za vijiji , mitaa , kata na halmashauri.


Ameeleza kuwa kwa takribani miaka 30 ya TGNP imekuwa mstari wa mbele katika kujenga uwezo na ushawishi juu ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia ikihusisha mchakato wa bajeti ya kila mwaka ili kuwawezesha wanawake na makundi yaliyo pembezoni katika ngazi za jamii kushiriki kikamilifu kupitia mchakato wa fursa na vikwazo (O&OD) unaofanyika katika ngazi za kijamii ili kuweza kuibua vipaumbele vyao.

Liundi ametoa rai kwa washiriki kutumia siku mbili za mafunzo kama fursa ya kujielimisha na kupata taarifa za kutosha ambazo zitawawezesha kushiriki katika mchakato wa kuhamashisha na kufuatilia utekelezajiwa bajeti katika ngazi za vijiji, mitaa, kata na halmashauri zetu kwa mrengo wa kijinsia.


Amewaasa washiriki kuwa maarifa watakayoyapata wataweza kuwashirikisha wananchi wengine katika maeneo wanayotoka ili kuwezesha ushiriki mpana wa wadau katika ufuatiliaji na kuhakikisha kuwa bajeti hiyo inatekelezwa ka namna ilivyopangwa hasa katika kutatua changamoto za makundi yaliyopembezoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na ufuatiliaji wa vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia kwa washiriki kutoka asasi za kiraia pamoja na vituo vya Taarifa na maarifa.
Baadhi ya washiriki kutoka vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Lilian Liundi alipokuwa anaiwasilisha kwa washiriki hao kwenye mafunzo ya siku mbili ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na ufuatiliaji wa vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia.
Mwezeshaji kutoka Idara ya Mafunzo na Ujengaji Uwezo wa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai akitoa elimu kuhusu mpango wa Bajeti yenye mrengo wa jinsia na ufuatiliani wa vituo vya Taarifa pamoja na asasi kwa washiriki kutoka asasi za kiraia na vituo vya Taarifa na maarifa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mtafiti na Mchambuzi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Zainabu Mmari akitoa mafunzo kwa washiriki asasi za kiraia na vituo vya Taarifa na maarifa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuhusu masuala ya jinsia na jinsia pamoja na kupanga Bajeti wakati wa mafunzo ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na ufuatiliaji wa vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia.
Baadhi ya washiriki kutoka vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia wakijadiliana kwenye makundi ili kuja na masuluhisho kwenye masuala ya usawa wa kijinisa kwenye mafunzo ya ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na ufuatiliaji wa vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia.
Mratibu wa Vituo vya Taarifa na maarifa Jacqueline Mtesha akiongoza washiriki kutoka vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia kuimba nyimbo mbalimbali wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa washiriki asasi za kiraia na vituo vya Taarifa na maarifa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini
Baadhi ya washiriki kutoka vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia wakichangia mada kwenye mafunzo ya ya Bajeti yenye mrengo wa kijinsia na ufuatiliaji wa vituo vya Taarifa na maarifa pamoja na asasi za kiraia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com