Na Marco Maduhu, SHINYANGA
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, imembana Mkandarasi kutoka Kampuni ya Brampem Global Investment LTD, kurudia matengenezo ya barabara aliyojenga chini ya kiwango, pamoja na kukatwa fedha kutokana na kuchelewesha matengenezo hayo kinyume cha Mkataba, huku ikitatua kero ya ukosefu wa madawa na vifaa tiba zahanati ya Kisuke halmashauri ya Ushetu.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja, amebainisha haya leo Agost 24, 2023 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kipindi cha robo ya Nne ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema kwa kipindi hicho walifanya ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya matengenezo ya barabara, zilizopo katika Manispaa ya Shinyanga chini ya usimamizi wa TARURA ili kuona utekelezwaji wa miradi hiyo kama imezingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.
Amesema katika ufuatiliaji wa matengenezo ya barabara hizo kwa uboreshaji wa vipande vya barabara katika Kata ya Chamaguha, Ngokolo, Ndembezi, Kambarage na Mwasele, walibaini Mkandarasi kutekeleza ujenzi wa barabara hizo chini ya kiwango.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
“Mkandarasi huyu kutoka Kampuni ya Brampem Global Investment mbali na uchelewashaji wa ukamilishaji wa mradi, ametekeleza kazi chini ya kiwango kwa kutochonga barabara kwa usahihi, kina chatabaka la kifusi kutofika kiwango na kutoshindiliwa ipasavyo, na uchongaji wa Mitaro isiyoridhisha,”amesema Masanja.
Aidha, amesema Mkandarasi huyo kwa sasa yupo kwenye kipindi cha makato ya fedha ikiwa ni adhabu ya kuchelewesha mradi kwa mujibu wa Mkataba, kwamba alipaswa akamilishe mradi huo Aprili 27 mwaka huu lakini licha ya kuongezewa siku 75 bado mradi huo wa matengenezo ya barabara haukukamilika.
Amesema Takukuru ilimshauri msimamizi wa mradi wa matengezo ya barabara hizo ambaye ni Tarura, imtake Mkandarasi arudie kazi zote alizotekeleza chini ya kiwango ili thamani ya fedha ionekane, na ushauri huo ulifanyiwa kazi na mpaka sasa marekebisho yamefanyika yenye thamani ya Sh.milioni 76 na thamani nzima ya mradi ni Sh.milioni 236.6.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Masanja amesema miradi mingine ya maendeleo ambayo waliifuatilia yenye thamani ya Sh.bilioni 5.6 katika Sekta ya Elimu, Maji, Kilimo na Ujenzi. walibaini kuwapo na dosari ndogo ndogo kwenye miradi miwili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Ibadakuli na Shule mpya ya Msingi Igaga na kurekebishwa.
Katika hatua nyingine amesema kupitia Proramu ya Takukuru Rafiki, walipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kata ya Kisuke Halmashauri ya Ushetu juu ya ukosefu wa vifaa tiba na madawa katika Zahanati ya Kisuke, na ukosefu wa Maji kwenye vijiji vya Ididi na Mutongi, na kero hizo zilifanyiwa kazi na wananchi kupata huduma.
Amesema kwa upande wa dawati la uchunguzi kwa kipindi hicho walipokea taarifa 35 za malalamiko, zilizohusu rushwa ni 26 na zinatoka katika Sekta mbalimbali, Elimu rushwa 7, Serikali za Mitaa 6,Ardhi 5, Polisi 2, Afya 2, Maji Moja na GPSA Moja, na uchunguzi wa taarifa hizo unaendelea.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kuendela kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo kwa kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya rushwa au ubadhilifu wa fedha kwenye miradi ya maendeleo ili hatua zichukuliwe.