*Dkt. Biteko asema biashara nyingi Sekta ya Madini inafanywa na India
Arusha
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Serikali ya Tanzania na nchi ya India umeimarika na umeendelea kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi.
Dkt. Biteko amesema hayo katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 77 ya Uhuru wa India zilizoandaliwa na watanzania wenye asili ya nchi hiyo yaliyofanyika Agosti 19 jijini Arusha.
"Kama mnavyofahamu nchi ya India na Tanzania zimekuwa na mahusiano ya muda mrefu ya kidiplomasia kiuchumi na jamii ya wahindi katika nchi yetu inajishughulisha na uwekezaji mwingi katika biashara na viwanda," amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema nchi ya India imefanya biashara nyingi kwenye Sekta ya Madini ikiwa pamoja na uuzaji na ukataji wa madini na mnyororo mzima wa shughuli uongezaji thamani madini.
Amesema hapa nchini wapo watu wenye asili ya India wapatao elfu 50 na kati ya hao wageni wenye pasipoti ya India wapo kati ya elfu 15 na elfu 20 na Arusha pekee ina zaidi ya watu 2000 wenye asili ya India na wamewekeza kwenye maeneo mengi na kufanya biashara mbalimbali.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, wageni wanaofika nchini kutoka India wamekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza na kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara kwenye Sekta ya Madini, viwanda na maeneo mengine.
"Tumeungana nao kusheherekea uhuru wao na kuwatia moyo, kuwatakia kila la heri kama Serikali tunawaunga mkono kwenye kila juhudi wanazozifanya na tunaliombea mema Taifa la India liendelee kuimarika ni Taifa kubwa lenye watu wengi na mchanganyiko mkubwa wa utamaduni," amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema Tanzania imekua sehemu salama pa kuishi na kufanya biashara na kuendeleza shughuli za utamaduni za nchi yao. Ameongeza kuendelea kuimarisha ushirikiano huo katika nyanja zote.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo amesema anajivunia umoja, upendo na mshikamano uliopo kati ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi hapa nchini hususan wanavyochangia katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
"Ukiangalia kwenye ajira wametoa ajira nyingi kwenye viwanda, lakini pia wanalipa kodi kwa Serikali. Nawaahidi kuwapa ushirikiano jamii ya Wahindi ili shughuli zao ziweze kuwa salama zaidi," amesema Gambo.
Nchi ya India huadhimisha sherehe za Uhuru kila ifikapo tarehe 15 Agosti ya kila mwaka ambapo jamii ya wahindi nchini pia imeadhimisha sherehe hizo mkoani Arusha.
Social Plugin