Lagos, Nigeria. Tarehe 1 Agosti 2023: Taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini, Benki ya CRDB imenyakua tuzo nne za kimataifa za umahiri katika ugavi zijulikanazo kama Africa Procurement and Supply Chain Awards (APSCA) 2023 jijini Lagos nchini Nigeria.
Benki yenyewe imeshinda tuzo mbili huku viongozi wake nao wakinyakua tuzo mbili kwa kutambua mchango wao katika kusimamia na kuongoza taratibu na viwango vya ununuzi na ugavi.
Katika hafla hiyo iliyo iliyofanyika katika Hoteli ya Oriental, Benki ya CRDB imenyakua tuzo ya umahiri katika ubunifu kwenye ununuzi na ugavi (sekta ya benki) na tuzo ya taasisi yenye idara bora ya ununuzi na ugavi. Pia, Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdulmajid Nsekela akitambuliwa kama Afisa Mtendaji Mkuu Anayewezesha vyema Idara ya Ununuzi na Ugavi huku Mkuruguzi wa Ununuzi wa Benki ya CRDB, Pendason Philemon, akitunukiwa tuzo ya mchango mkubwa kwenye taaluma ya ununuzi na ugavi katika sekta ya benki akiwa miongoni mwa viongozi 50 wa eneo hilo waliotambuliwa katika awamu hii ya tano ya APSCA.
Akipokea tuzo kwa niaba ya Nsekela, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt Benson Bana amesema ni furaha kubwa kwake kuungana na Watanzania wenzake, hasa wafanyakazi wa Benki ya CRDB ambayo imeliheshimisha taifa kwa kushinda tuzo nne za umahiri katika ununuzi.
“Naipongeza sana Benki ya CRDB, viongozi na wafanyakazi wake hasa Bwana Abdulmajid Mussa Nsekela ambaye amepewa tuzo ya Afisa Mtendaji Mkuu anayewezesha vyema Idara ya Ununzi na ndugu yangu Philemon ambaye amezawadiwa tuzo ya juu katika masuala ya ununuzi. Ni heshima kwa Watanzania, Benki ya CRDB imetuweka mbele na kutuheshimisha na imeendelea kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kuifungua nchi kwani Tanzania sasa inasikika Nigeria na imesikika Afrika na sio kusikika tu bali kuzoa tuzo katika eneo la ununuzi kimataifa,” amesema Balozi Bana.
Tuzo za APSCA huwatambua wataalamu, idara na taasisi zenyeumahiri, mchango au umakini mkubwa katika kuzingatia viwango vya hali ya juu katika ununuzi na ugavi kimataifa. Hili linafanywa kwa imani kwamba ununuzi unaozingatia viwango vya kimataifa ni muhimu kwani unaweza kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza ufanisi wa taasisi na jamii kwa ujumla.
Akielezea ushindi uliopatikana, Philemon amesema kila mwaka APSCA hutoa tuzo hizo, lakini Benki ya CRDB imeshiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu ambao umeshuhudia washiriki 83 wakichuana na Benki kuibuka kidedea tena kwa kishindo.
“Ilikuwa furaha na fahari ya aina yake kwa benki yetu kuitwa jukwaani mara nne kwenda kupokea tuzo za umahiri mbele ya mamia ya wataalamu wa fani ya ununuzi na ugavi. Ulikuwa usiku mzuri kwa Benki ya CRDB na kampuni ya mawasiliano ya MTN ya nchini Nigeria tuliong’ara Zaidi kwa kupata tuzo nyingi, nne kila taasisi. Tuzo hizi zinadhihirisha uwezo mkubwa wa Watanzania kwamba tunaweza kushindana kimataifa na kutoka kimasomaso hivyo tujielekeze kupambana na wenzetu kutoka popte duniani,” amesema Philemon.
Kwa upande wake, Nsekela amesema usimamizi wa ununuzi na ugavi ni suala nyeti ambalo ni zaidi ya kuhamisha bidhaa kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mteja.
“Kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa sawia, kunahitaji jicho makini la menejimenti. Bila idara imara ya ununuzi na ugavi, benki haiwezi kutoa huduma bora kwa wateja wake. Mchango wa idara hii unajenga msingi wa mafanikio ya benki katika maeneo mbalimbali. Nimefuahi kuona idara yetu ununuzi na ugavi pamoja na menejimenti yake ikitambuliwa kutokana na umahiri wake kwa kuzingatia kanuni zinazotakiwa na kukubalika duniani kote. Naahidi nitaendelea kuipa ushirikiano kadri itakavyohitajika,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba Bara la Afrika kwa sasa linatekeleza mkataba wa eneo huru la biashara unaoruhusu biashara, bidhaa na huduma kufanyika bila mipaka na pia raia wa kiafrika kuvuka mipaka bila vikwazo hivyo kufungua soko la zaidi ya watu bilioni 1.3. Ili kulihudumia kiushindani soko hili, kampuni na taasisi zinapaswa kufanya biashara na kutoa huduma kwa kuzingatia vigezo na viwango vya kimataifa.
“Benki ya CRDB inakusudia kutoa huduma zake kwa watu wengi katika soko hili kubwa. Hilo litafanikiwa kwa kuwa Benki inajikita katika umahiri wa kutoa huduma viwango vya kimataifa. Tuzo hizi tulizoshinda ni uthibitisho kwamba huduma zetu ni za kiwango kikubwa zinazolenga kukidhi malengo na matarajio ya wateja wetu,” amesisitiza Nsekela.
Kwa miaka minne mfululizo, tuzo za APSCA zilikuwa zinafanyika nchini Ghana. Zikifanyika nchini nigeria mwaka huu, tuzo hizo zimeandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Ununuzi na Usimamizi wa Ugavi (CISCM)), Taasisi ya Ununuzi na Ugavi Ghana (GIPS) na Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Nigeria (APPON).--
Social Plugin