Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEC: AJIRA ZA WATENDAJI WA UCHAGUZI ZIZINGATIE SIFA NA UWEZO


Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufaa (Mstaafu) Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maafisa uchaguzi mkoani Morogoro leo tarehe 10 Agosti, 2023.
Sehemu ya wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maafisa uchaguzi wakimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati akifunga mafunzo hayo Mkoani Morogoro leo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewakumbusha Wasimamzi wa Uchaguzi kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba ajira za watendaji wa uchaguzi zinazingatia sifa na uwezo.


Ukumbusho huo umefanywa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufaa (Mstaafu) Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk mkoani Morogoro leo tarehe 10 Agosti, 2023 wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maafisa uchaguzi.


Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu na kuhudhuriwa na washiriki 88 ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara.


“Tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hii muhimu, jambo hili limekuwa likisisitizwa tokea siku ya kwanza ya mafunzo kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni. Kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika kuitekeleza,” amesema Jaji Mbarouk.


Amesisitiza juu ya kuhakikisha kwamba mafunzo kwa watendaji wa vituo vya kupigia kura yanafanywa kwa ufanisi ili wawe na uelewa na kuweza kufanya kazi zao kwa usahihi na kujiamini.


“Ni imani yetu kuwa mafunzo ya watendaji wa vituo yatafanyika kwa ufanisi na weledi katika tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo ili waweze kufahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo wakati wa uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.


Aidha, amewahimiza watendaji wa uchaguzi kutenga muda kujisomea ili kupata ufahamu wa sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


“Natumia nafasi hii kuendelea kuwasisitiza kuhusu umuhimu wa kutenga sehemu ya muda wenu kusoma Katiba, Sheria na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki,” amesema.


Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023, wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.


Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com