Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Katika mchezo huo, Simba SC wameibuka kidedea kwa jumla ya mikwaju ya penalti 3-1 dhidi ya mtani wao Yanga SC baada ya sare ya 0-0 kwenye dakika 90’ za mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki lukuki wa soka kwenye dimba hilo la Mkwakwani.
Changamoto ya mikwaju ya penalti ilifuata baada ya sare hiyo tasa kwenye dakika hizo 90’. Simba SC walianza kupiga mkwaju wao wa penalti kupitia kwa Kiungo wao, Mzamiru Yassin Selemba ambaye alimpoteza maboya Golikipa wa Yanga SC, Djigui Diarra.
Yanga SC walipiga mkwaju wao wa kwanza kupitia kwa Stephane Aziz Ki ambaye alipiga vizuri mkwaju huo na kuweka wavuni akimuacha Golikipa Ally Salim hana la kufanya. Simba SC walipiga mkwaju wao wa pili kupitia kwa Saido Ntibazonkiza ambaye alikosa kwa Diarra kupangua vizuri.
Kiungo Khalid Aucho alikosa mkwaju wa penalti wa pili baada ya Ally Salim (The hero) kudaka na kuuficha kabisa mpira wa Aucho uliopigwa upande wake wa kulia. Simba SC nao walikosa mkwaju wa tatu baada ya Moses Phiri kuupeleka juu ya lango mpira.
Mkwaju wa tatu wa penalti wa Yanga SC uliopigwa na Kiungo Pacôme Zouzoua ambaye alikosa kwa mkwaju wake kupanguliwa na Ally Salim. Penalti ya nne ya Simba SC ilipigwa na Mshambuliaji Onana Essomba Willy ambaye alipata kwa kumuacha Kipa Diarra hana la kufanya.
Mlinzi wa kulia wa Yanga SC, Kouassi Attohoula Yao alikosa mkwaju wa nne ambao ulipanguliwa tena na Ally Salim. Mkwaju wa ushindi kwa upande wa Simba SC ulipigwa na Mshambuliaji Jean Baleke ambaye alimuacha Diarra hana la kufanya kudaka mkwaju huo.
Mchezo wa awali wa kusaka nafasi ya tatu wa Ngao ya Jamii uliisha kwa Azam FC kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Singida Big Stars kwenye huo huo wa CCM Mkwakwani.
Katika mchezo huo mabao ya Azam yalifungwa na Washambuliaji Prince Dube kwenye dakika ya 1’ na Abdul Suleiman Sopu dakika ya 42’.