Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd (wa pili kulia), akimkabidhi Robert Masala kadi ya gari aina ya Toyota Crown baada ya kushinda katika kampeni ya Benki ni SimBanking katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa mshindi, Goba jijini Dar es Salaam Agosti 17, 2023. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Meneja wa CRDB Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Donath Shirima na Balozi wa Benki ya CRDB Stephane Aziz Ki.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd (katikati), akimkabidhi namba ya gari aina ya Toyota Crown mteja wa benki hiyo, Robert Masala (wa pili kulia) baada ya kuibuka mshindi wa kampeni ya Benki ni SimBanking katika hafla ilifyoanyika nyumbani kwa mshindi huyo Goba jijini Dar es Salaam Agosti 17, 2023. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Meneja wa CRDB Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Donath Shirima, Balozi wa Benki ya CRDB, Stephane Aziz Ki na kulia ni Meneja Mwandamizi wa Huduma Mbadala za Kibenki, Mangire Kibanda.
========= ========= =========
Benki ya CRDB imemkabidhi Robert Masala, mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam gari jipya aina ya Toyota Crown baada ya kuibuka mshindi katika awamu ya tatu ya kampeni ya Benki ni Simbanking.
Masala aliyeibuka kidedea kwa mwezi Julai anaungana na Jared Awando Ojweke aliyekuwa mshindi wa shinda gari Juni na Mayani Yahaya Hassan aliyekuwa wa kwanza mapema Mei.
Akieleza namna anavyoitumia huduma za SimBanking, Masala amesema amekuwa mteja wa Benki ya CRDB tangu mwaka 2005 na huduma hiyo imekuwa ikimrahisishia kufanya miamala hasa ya biashara zake kwa urahisi na kwa wakati.
“Mimi ni mwajiriwa hapa Dar lakini nina biashara Mwanza ambako ndio nyumbani. Simbanking huwa inanisaidia sana kwenye usimamizi wa mapato na matumizi ya biashara. Kati ya mwezi Mei na Juni nilikuwa na miradi naikamilisha hivyo nilitumia sana Simbanking nje ya utaratibu wa kawaida. Nadhani hii imechangia kwa namna au nyingine mimi kushinda gari hili,” amesema Masala.
Tangu alipofungua akaunti ya Benki ya CRDB, Masala ambaye ni baba wa watoto wawili anasema amekuwa akitumia huduma za Simbanking tangu tangu mwanzoni ilipokuwa ikitumia teknolojia ya USSD pekee kwa kubofya *150*03# mpaka ilipoanzishwa programu ya kidijitali ya SimBanking App ambayo amesema ni rahisi na ina ufanisi mkubwa.
Kwa waajiriwa wenzake, Masala amewashauri kuitumia Benki ya CRDB pamoja na Simbanking ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda zawadi kemkem zinazotolewa kila mwezi kuanzia fedha taslimu, simu za mkononi hata gari hasa Toyota Crown linalotolewa kila mwezi na Vanguard atakalokabidhiwa mshindi wa jumla.
Kama ilivyokuwa kwa washindi waliomtangulia, Masele naye amekabidhiwa gari hilo lenye thamani ya TSZ 20 milioni likiwa limekatiwa bima kubwa na kujaziwa mafuta “full tank.”
Akimkabidhi zawadi hiyo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Mashariki, Badru Idd amesema kwa hali ilivyo sasa hivi ni ngumu kuuepuka uchumi wa kidijiti hivyo Watanzania hawapaswi kubaki nyuma watumia huduma za Simbanking, jukwaa bora zaidi nchini na linaloongoza kwa kutumiwa kati ya programu za benki zilizopo.
“Leo tunamtangaza Robert Masala aliyeibuka mshindi wa gari kwenye droo iliyochezeshwa tarehe 3 mwezi huu. Yeye ni ni mshindi wa tatu kuondoka na gari baada ya Jared Awando Ojweke wa hapa Dar es Salaam na Mayani Yahaya Hassan wa mkoani Dodoma kushinda miezi miwili iliyopita. Simbanking ni ya kila mtu, unaweza kumaliza mahitaji yako ukiwa mahali popote,” amesema Idd.
Ikiwa benki kiongozi nchini, meneja huyo amesema Benki ya CRDB inahakikisha wakati wote inaboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya wateja ikitambua kwamba matarajio yao yanabadilika kila siku.
Hivi karibuni Benki ya CRDB ilizindua SimBanking App mpya ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki katika kuboresha huduma na kuleta mapinduzi katika sekta ya fedha nchini.
SimBanking mpya imetengenezwa kwa muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili mnemba (Artificial intelligence), jambo linaloifanya kuwa na uwezo mkubwa katika utambuzi wa tabia na mahitaji ya mteja pindi anapotumia.
Mshindi wa gari aina ya Toyota Crown wa kampeni ya Benki ni Simbanking ya Benki ya CRDB, Robert Masala akiwa na mkewe, Esther Itule baada ya kukabidhiwa gari hilo na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Mashariki, Badru Idd.