Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YADHAMIRIA KUREJESHA MINADA YA MADINI, KUUZA TANZANITE NJE YA MIRERANI


*Dkt. Biteko Asema Kuna Makubwa Matumaini Sekta Kuchangia Asilimia 10 Katika Pato la Taifa Mwaka wa Fedha 2023/24

Dodoma

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema katika kuhakikisha biashara ya Tanzanite inafanyika nje ya eneo la Mirerani ili kuleta faida kwa nchi, Wizara ya Madini inatarajia kurejesha Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Arusha yatakayofanyika kila mwaka kulingana na kalenda za kimataifa ya maonesho ya madini ya vito na biashara za usonara.


Mhandisi Samamba ameyasema hayo Agosti 23, 2023 jijini Dodoma wakati akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini taarifa kuhusu hali ya Kituo cha Kuuuzia Madini ya Tanzanite na Mkakati wa kuuza Madini hayo nje ya eneo la Mirerani.


Ameongeza kuwa kwa sasa Wizara ipo kwenye mchakato wa kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho na minada ya vito kufanyika nchini ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya Tanzanite nje ya Mirerani.

"Uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa nchini Tanzania hususan Tanzanite katika masoko ya kimataifa ikiwa ni moja ya njia za kuwafikisha watanzania kwenye masoko ya uhakika ya kimataifa yanayotoa bei nzuri na stahiki za madini wanayozalisha,’’ amesema Mhandisi Samamba.


Akiitaja mikakati mingine ya kuimarisha biashara hiyo amesema, wizara imepanga kufanya minada ya ndani katika miji mbalimbali hususan madini ya Tanzanite katika mji wa Mirerani itakayohusisha wanunuzi kutoka mikoa mingine ya Tanzania ili kuchochea ukuaji wa miji husika, uzalishaji wa madini na upatikanaji wa bei shindani ya madini husika.

Pia, amesema wizara inatarajia kufanya minada ya kimataifa ya madini ya vito aina zote katika mji wa Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar na kila robo ya mwaka kutokana na miji hiyo kuwa na vivutio vya utalii na miundombinu ya hoteli na migahawa yenye viwango vya kimataifa na usalama wa kutosha.

Akizungumzia biashara ya Tanzanite, amesema katika kusimamia udhibiti na biashara ya madini kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 jumla ya leseni 28 za wafanyabiashara wakubwa na leseni 299 za wafanyabiashara wadogo zilitolewa ikilinganishwa na leseni 54 za wafanyabiashara wakubwa na leseni 244 za wafanyabiashara wadogo wa madini zilziotolewa Mwaka wa Fedha 2021/22.


Aidha, ameieleza kamati hiyo kwamba , kupungua kwa idadi ya leseni za wafanyabiashara kulitokana na kuimarishwa kwa usimamizi na udhibiti katika biashara ya madini hayo kufuatia tamko la Serikali la kuhamishia biashara ya Tanzanite ya Mirerani.


Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika kikao hicho amesisitiza kuwa wizara ilifanya uchambuzi wa kina ili kubaki na wafanyabiashara wachache wanaofanya shughuli zao vizuri na zenye tija kwa taifa.


Ameongeza kwamba, Wizara inaendelea kupambana kuhakikisha inaongeza thamani ya madini ya Tanzanite ambayo ni madini yanayozalishwa Tanzania pekee duniani kote.

Akizungumzia umuhimu wa maonesho hayo amesema yatasaidia kuvutia wanunuzi wakubwa ikiwemo kuwawezesha wachimbaji kunufaika kutokana na bei kuwa za uhakika.


Dkt. Biteko ameongeza kwamba, Sekta ya madini imeendela kuwa kinara katika kuliingizia taifa fedha za kigeni kutokana na bidhaa za madini zinazouzwa nje ya nchi na kueleza kwamba kutokana na mwenendo mzuri Sekta ya Madini, asilimia 10 ya mchango wake kwenye Pato la Taifa unaweza kufikiwa katika mwaka huu wa Fedha wa 2023/24 tofauti na Mwaka 2025 kama ilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025.


Naye, Mwenyekiti wa Kamati wa Kudumu ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula ameendelea kulipongeza Shirika la Madini la taifa STAMICO kwa namna lilivyopiga hatua na kuchangia katika maendeleo ya Sekta ya Madini na hivyo, kuitaka Wizara kuendelea kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yanayotolewa na kamati hiyo kwa maendeleo ya Sekta ya Madini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com