Kamishana wa Kamisheni ya Ushirikishwaji Jamii CP Faustine Shilogile leo Jumamosi Agosti 05, 2023, amefanya ziara ya kukagua miradi ya Polisi jamii mkoani Shinyanga ikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi ili kuweza kushirikiana katika kuzuia na kutokomeza uhalifu mkoani Shinyanga.
Akiongea na wakuu wa himaya katika ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Kamishna Shilogile amewataka wakuu hao wa himaya kuwatumia vizuri askari kata katika maeneo yao kwani askari hao ndiyo tegemeo la Jeshi katika kupambana na uhalifu nchini.
Kamishna Shilogile amewasisitiza wakuu wa himaya kwamba, Polisi Jamii ndiyo Uti wa mgongo wa Jeshi la Polisi, hivyo kila mkuu wa himaya ni lazima ahakikishe kwamba anatumia nguvu zake zote na weledi katika kuimarisha ustawi wa Polisi Jamii katika himaya yake.
Katika ziara hiyo, Kamishna Shilogile ameambatana na mratibu wa dawati la jinsia na watoto ACP- Faidha Suleiman ambaye kwa upande wake amezungumzia umuhimu wa kuwatumia askari wenye nguvu na elimu katika saikilojia ya ushauri katika kuhudumia wahanga mbalimbali wanaohitaji huduma za dawati.
Hata hivyo Acp Faidha amesisitiza kutumia Askari wenye weledi katika madawati ya Jinsia kwani idara hiyo inahitaji umakini mkubwa katika kutatua changamoto za wahanga.
Naye Kamishna mstaafu WA Jeshi la Polisi Rt Sacp Englibert Kiondo amesisitiza na kuhamasisha uwepo wa askari wa kata katika kila himaya huku akitoa mifano iliyo hai kuhusiana na umuhimu wa Polisi Jamii katika himaya zetu.
Kamishna Shilogile amepata wasaa wa kutembelea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga na kuongea na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa, akiwa ofisini hapo, Kamishna Shilogile alitoa historia fupi ya Polisi Jamii huku akisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwake na namna ambavyo Jeshi la Polisi linavyokabiliana na uhalifu kwa kushirikiana na wananchi.
Akitoa mchango wake, mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mh. Mdeme alimpongeza na kumwagia maua yake Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi kwa juhudi kubwa ya kuzuia uhalifu mkoani Shinyanga.
"Najivunia kuwepo kwa Kamanda Magomi hapa mkoa wa Shinyanga, hali ya uhalifu imeshuka sana, siku hizi unaweza kukaa wiki nzima usisikie tukio lolote baya",amesema Mhe. Mndeme.
Mkuu wa mkoa amebainisha kwamba mafanikio hayo yote yametokana na Ushirikishwaji wa Jamii katika kuzuia uhalifu.
Pia mkuu Mkoa, amemshukuru mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Wambura kwa kuwapatia gari jipya Polisi wilaya ya Msalala ambalo limerahisisha utendaji kazi.
Akihitimisha ziara hiyo ndani ya wilaya ya Shinyanga, Kamishna Shilogile amepata wasaa wa kuongea na viongozi mbalimbali wa Serikali za mitaa na madiwani wa wilaya ya Shinyanga lakini pia vikundi mbalimbali vya ulinzi shirikishi.
Social Plugin