Fundi mwandamizi kutoka kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) Jeremia Simoni akionesha wananchi waliohudhuria katika maonesho ya nane nane yanayofanyika katika viwanja vya Themi nane nane njiro mkoani Arusha namna mashine ya kufunga majani inavyofanya kazi
Na Woinde Shizza , ARUSHA
Kutokana na tatizo la ukosefu wa malisho ya mifugo haswa katika kipindi cha ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi ,kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) kimemletea mkulima suluhisho kwa kumtengenezea mashine itakayomsaidia kukata, kufunga majani kwa ajili ya kuhifadhi malisho yatakayomsaidia katika kipindi ambacho hakuna mvua na malisho hayapatikani pamoja na kumwezesha mkulima kujipatia kipato.
Akiongea na waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima yanayofanyika kufanyika katika viwanja vya nane nane Themi Njiro mkoani Arusha ofisa masoko kutoka taasisi hiyo James Joseph alisema kuwa katika msimu huu wa nane nane wameamua kuwaletea wafugaji teknolojia hizo ili kuweza kupunguza tatizo kubwa la chakula cha mifugo linalowakabili wafugaji wengi hapa nchini pamoja na kumsaidia mkulima katika njanja za biashara.
Alisema kuwa tatizo la ukame linalotokea hapa nchi limekuwa likipelekea kukosekana kwa malisho ya mifugo hivyo mashine hizo zitamuwezesha mfugaji kuhifadhi chakula kinachotokana na mazao mbalimbali yanayovunwa katika kipindi cha mavuno na kuhifadhiwa vyema kwa ajili ya kusaidia katika kipindi cha ukame.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka iliyopita kumekuwa na tatizo la chakula cha mifugo ambalo linatokana na changamoto ya kutokuwepo kwa mvua , ambapo inapelekeaga mifugo mingi kupoteza maisha .
"Kupitia mashine hizi ambazo tumewaletea wakulima na wafugaji wanaweza kufaidika katika njia mbalimbali kwa mfano yale mabua ambayo wakulima walikuwa wakiyapata kutokana na mavuno walikuwa wakisafirisha kwa gharama kubwa sana kwa mfano mfugaji akikodi kenta Moja ambayo inaweza kubeba tani nne anaweza kusafirisha majani kidogo sana kwa gharama ya kiasi cha shilingi laki tatu ,lakini pia akifikisha yale majani sio yote yatalika na mifugo kutokana na kuharibika kiasi ambacho zaidi ya asilimia 90% ya yale mabua ng'ombe hayali yakifika katika eneo la kuhifadhia lakini akitumia njia hii badala ya ng'ombe kula asilimia 20 ya majani na nyingine kupotea lakini kwa kupitia njia hii mfugo huyo atakula majani
kwa asilimia 90 yote",alisema.
Alisema kupitia teknolojia hizo zitamsaidia mkulima kuokoa chakula cha mifugo kwa zaidi ya asilimia 90% ,pia zitamsaidia mfugaji kuhifadhi chakula kingi cha mifugo katika eneo dogo kitakacho muwezesha kuilisha mifugo yake katika kipindi chote ambacho kitakuwa na tatizo la chakula cha mifugo.
Aliwataka watanzania kuwekeza katika chakula cha mifugo kwani kinalipa na hakuna watu wengi kama vile ,zilivyo biashara zingine.
Aidha aliwataka wakulima nchini kubadilika na kuachana na ufugaji wa mazoea bali wafuge kisasa kwa ajili ya kupata mazao mengi lakini yenye ubora ambayo yataweza kuuzika kwa faida na hivyo kuongeza mchango wa pato la Taifa.
Alisema ufugaji wa kisasa unaleta manufaa makubwa hata ukiwa na mifugo michache ambayo utaitunza vizuri tofauti na kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo haikusaidii kuinuka kiuchumi ambayo pia itakufanya ushindwe kuilisha kutokana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.