COSTECH KUENDELEA KUSIMAMIA KIGODA CHA UTAFITI SUA NA NM-AIST


Na Dotto Kwilasa,Dodoma.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH)imesema inaendelea kusimamia miradi mbalimbali ukiwemo wa Kigoda cha Utafiti katika SUA na NM-AIST ambao ni wa miaka mitano, wenye thamani ya takribani shilingi bilioni Tano.

Aidha inaendelea kushirikiana na Mabaraza ya Kikanda na Kimataifa kuhakikisha fursa zinapatikana ikiwa ni pamoja na kusaidia kuleta fedha za utafiti kupitia COSTECH au kuhamasisha Taasisi za ndani kuomba hizo fursa.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo ,Agosti 25,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Dkt.Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli na mafanikio ya tume hiyo.

Dkt.Nungu ametaja baadhi ya shughuli zilizotekelezwa na Tume hiyo kuwa ni pamoja na kuibua na kufadhili miradi ya kimkakati ambayo tayari michakato yake imefanyika na sasa ipo katika hatua ya mikataba ambapo Serikali kupitia COSTECH imeidhinisha jumla ya miradi saba kwa thamani ya shilingi milioni 150 kila mradi.

Amesema Miradi hiyo itafanyika ndani ya miaka miwili na inahusisha watafiti na wabunifu kutoka sekta zote za umma na binafsi.

Aidha amesema kuwa Serikali kupitia COSTECH, imeidhinisha miradi miwili kwa thamani ya shilingi milioni 120 kila mradi ambapo utekelezaji wake pia unahusisha watafiti kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini na itafanyika ndani ya miaka miwili, sasa ipo hatua ya kusaini mikataba.

Amesema,"Serikali ilifadhili miradi ya utafiti kupitia COSTECH, baadhi ya miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Tume inafanya ufuatiliaji wa miradi inayohusu kuboresha maabara za utafiti kwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa ikiwemo, Maabara ya Utafiti wa Baharini katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mradi ambao tayari ulishakamilika,”amesema Dkt.Nungu

Akizungumzia majukumu na vipaumbele vya tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Dkt.Nungu amesema kuwa Tume hiyo COSTECH yafadhili mradi utafiti matokeo mabaya somo la hisabati kidato cha nne na darasa la saba.

“Somo la hisabati bado linaonekana ni changamoto kwani matokeo yake yamekuwa mabaya Kwa kidato cha nne na Darasa la nne hivyo kwa kubaini chanzo cha tatizo hilo sisi kama Tume tumeidhinisha miradi miwili ambayo kila mmoja thamani yake ni milioni 120,”amesema Dkt.Nungu



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post