Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wapili kutoka kushoto) akiangalia baadhi ya mifugo iliyopo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya). Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi.
Na Edward Kondela
Serikali imewaasa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kujisajili na kushiriki vyema katika Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika 2023 (AGRF) ili waweze kufungua fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (06.08.2023) katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, ambapo amesema tayari wizara imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhamasisha wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kushiriki katika mkutano huo ambao utafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 8 Mwezi Septemba mwaka huu na unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Mhe. Ulega amesema mkutano huo wa Afrika utakaofanyika jijini Dar es Salaam unatarajia kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kuongeza wigo wa mawasiliano ya kibiashara kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” BBT – LIFE kwa ajili ya kuwezesha vijana kupata elimu ya vitendo katika unenepeshaji wa mifugo na viumbe vya kwenye maji, Waziri Ulega amebainisha kuwa programu hiyo inafanyika kutokana na maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo hadi sasa takriban vijana 240 wapo kwenye mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa vijana wanashirikishwa katika hatua zote ikiwemo ya kujenga mabanda na kwenda minadani na kuchagua ng’ombe wazuri ambao wanaweza kunenepeshwa na namna hatua za unenepeshaji zinavyofuatwa ambapo hadi sasa ng’ombe 500 wameuzwa.
Aidha, amesema programu hiyo ilivyo ni kwamba tangu siku ya kwanza kila kijana anajua idadi ya ng’ombe atakaowasimamia na kila anapowauza ule mzunguko faida inayobaki ndiyo atakayoondoka nayo kuanzisha biashara yake na upande wa uvuvi imetolewa elimu juu ya unenepeshaji wa kaa na jongoo bahari pamoja na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Pia, amesema matumaini ni kwamba Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” ni kupanua zaidi program hiyo na kuishusha katika ngazi ya mkoa na wilaya ili ziweze kujiendesha pamoja na kuongeza kundi la vijana kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili wapate pia mafunzo hayo.
Kuelekea Uchumi wa Buluu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), amesema serikali inaenda kuwezesha wavuvi wadogo wadogo kuingia kwenye maji marefu ili waweze kufanya huko shughuli za uvuvi.
Waziri Ulega amebainisha kuwa wavuvi hususan wadogo watawezeshwa boti kupitia mikopo isiyo na riba sambamba na kutumia fursa za uchumi wa buluu kwa kunenepesha jongoo bahari na kilimo cha mwani pamoja na uwepo wa vizimba vya kufugia samaki lengo ni kuongeza uzalishaji kupitia uchumi wa buluu kwa kuwa na ongezeko la samaki katika soko la ndani na nje ya nchi.
Social Plugin